Ni ipi hukumu ya kukusanyika karibu na kaburi kwa ajili ya kisomo cha Qur-aan?

Swali: Ni ipi hukumu ya kukusanyika karibu na kaburi kwa ajili ya kisomo cha Qur-aan? Je, maiti ananufaika na kile kisomo?

Jibu: Kukusanyika karibu na kaburi na kusoma Qur-aan ni maovu ambayo hayakuwepo wakati wa Salaf.

Kuhusu kama maiti ananufaika, ikiwa makusudio ni kwamba maiti yule asikie, hili halipo. Kwani maiti yule ameshakufa. Imethibiti ya kwamba Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Anapofariki mwanadamu matendo yake yote yanakatika isipokuwa mambo matatu; swadaqah yenye kuendelea, elimu watu wananufaika kwayo au mtoto mwema anayemuombea.”[1]

Hata kama tutasema kuwa anasikia katika hali hii, bado hanufaiki. Angenufaika basi matendo yake pia yasingelikatika. Hadiyth imesema wazi ya kwamba maiti ananufaika kwa matendo yake matatu tu yaliyotajwa. Ikiwa makusudio ni kwamba maiti ananufaika na kile kisomo cha msomaji kwa njia ya kwamba msomaji ananuia thawabu za kisomo zimwendee yule maiti, tukisema kuwa kitendo hichi ni Bid´ah, basi hakuna thawabu katika Bid´ah. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Ninakutahadharisheni na Bid´ah, kwani hakika kila Bid´ah ni upotevu na kila upotevu ni Motoni.”[2]

Hatuwezi kugeuza upotevu ukawa ni uongofu.

Isitoshe mara nyingi visomo hivi vinakuwa kwa malipo. ´Ibaadah kwa malipo ni batili. Yule mkodishwaji na anataka kulipwa thawabu hapa duniani kwa udhahiri wa matendo mema hanufaiki nayo; hayamkufurisha mbele ya Allaah na wala hapewi ujira kwayo. Allaah (Ta´ala) amesema:

مَن كَانَ يُرِيدُ الْحَيَاةَ الدُّنْيَا وَزِينَتَهَا نُوَفِّ إِلَيْهِمْ أَعْمَالَهُمْ فِيهَا وَهُمْ فِيهَا لاَ يُبْخَسُونَ أُوْلَئِكَ الَّذِينَ لَيْسَ لَهُمْ فِي الآخِرَةِ إِلاَّ النَّارُ وَحَبِطَ مَا صَنَعُواْ فِيهَا وَبَاطِلٌ مَّا كَانُواْ يَعْمَلُونَ

” Anayetaka uhai wa dunia na mapambo yake Tutawalipa kikamilifu matendo yao humo nao hawatopunjwa chochote humo – hao ndio wale ambao hawatokuwa na chochote Aakhirah isipokuwa Moto na yataharibika yale waliyoyafanya humo na ni yenye kubatilika yale waliyokuwa wakiyatenda.”[3]

Msomaji huyu ambaye amenuia kwa kisomo chake kupata maslahi ya kidunia anatakiwa kutambua kuwa kisomo chake hakikubaliwi na ni chenye kubatilika. Kwa vile kitendo hicho hakina thawabu yoyote basi yule maiti hapewi thawabu kwacho. Kwa msemo mwingine kitendo hicho ni kuharibu mali na wakati huo huo ni kutoka nje ya njia ya Salaf (Radhiya Allaahu ´anhum) na khaswa ikiwa mali hii ni katika mirathi ya yule maiti. Mali hii ni haki ya wachanga, watoto na ambao hawajakomaa. Kuharibu mali yao pasi na haki kunaifanya dhambi iwe kubwa na mbaya zaidi.

[1] Muslim (1631).

[2] Abu Daawuud (4607), at-Tirmidhiy (2676) na Ibn Maajah (34). Swahiyh kwa mujibu wa al-Albaaniy katika ”al-Irwaa’” (2455).

[3] 11:15-16

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Majmuu´-ul-Fataawaa (17/224-226)
  • Imechapishwa: 02/09/2021