Ni ipi hukumu ya kumpa maiti thawabu za kisomo?

Swali: Ni ipi hukumu ya kumtumia maiti thawabu za kisomo cha Qur-aan?

Jibu: Kitendo hichi kinapitika kwa njia mbili:

1 – Mtu akaenda kwenye kaburi la maiti na akamsomea. Haya hayamnufaishi yule maiti. Usikilizaji unaomnufaisha ni ule unaopitika katika uhai wake. Wanapewa thawabu wote wawili yule msikilizaji na yule msomaji. Katika hali hii maiti matendo yake yamekatika. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Anapofariki mwanadamu matendo yake yote yanakatika isipokuwa mambo matatu; swadaqah yenye kuendelea, elimu watu wananufaika kwayo au mtoto mwema anayemuombea.”[1]

2- Mtu akasoma Qur-aan tukufu kwa ajili ya kumuabudu Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala) na wakati huo huo akamtumia thawabu za kisomo ndugu yake na jamaa yake muislamu. Wanachuoni wametofautiana juu ya kitendo hichi:

1 – Kuna wenye kuonelea kuwa matendo ya kimwili hayamnufaishi yule maiti hata kama atapewa thawabu zake. Asli ni kuwa ´ibaadah imefungamana na yule mwenye kuifanya. ´Ibaadah ni ibara ya unyenyekevu na kufanya maamrisho, jambo ambalo linamrudilia yule mtendaji peke yake. Isipokuwa yaliyothibiti kwa dalili na kwa hiyo hayo ni maalum.

2 – Wanachuoni wengine wanaonelea kuwa zile dalili zinazoonyesha thawabu za baadhi ya matendo zinamfikia maiti ni dalili kwamba thawabu za matendo mengine yote zinamfikia pia maiti.

Kilichobaki ni kuangalia kama jambo hilo ni katika mambo yaliyowekwa katika Shari´ah au ni katika mambo yenye kujuzu. Kwa msemo mwingine, imependekezwa mtu kusoma Qur-aan tukufu na kumtumia thawabu zake jamaa au ndugu muislamu maiti au ni katika mambo yenye kujuzu peke yake na halikupendekezwa? Naonelea kuwa ni katika mambo yenye kujuzu peke yake na halikupendekezwa. Yaliyopendekezwa ni kumuombea du´aa na msamaha yule maiti na mfano wa hayo. Kufanya matendo mema na kupeana thawabu zake kubwa linaloweza kusemwa ni kuwa inajuzu tu. Ni jambo halikupendekezwa. Kwa ajili hii Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) hakuwapendekezea nalo Ummah wake. Badala yake aliwapendekezea Ummah wake wamuombee du´aa maiti. Ni dalili inayoonyesha kuwa du´aa ni bora zaidi kuliko kumpa thawabu.

[1] Muslim (1631).

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Majmuu´-ul-Fataawaa (17/226-227)
  • Imechapishwa: 02/09/2021