Ni ipi hukumu ya kukodi watu nyumbani waje kumsomea yule maiti?

Swali: Ni ipi hukumu ya kusoma Qur-aan kwenye kaburi baada ya mazishi? Ni ipi hukumu ya kukodi nyumbani watu wataomsomea yule maiti Qur-aan?

Jibu: Maoni yenye nguvu ya wanachuoni ni kwamba kusoma Qur-aan kwenye kaburi baada ya mazishi ni Bid´ah. Kitendo hicho hakikukuwa katika zama za Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Hakukiamrisha na wala hakuwa akikifanya. Kubwa lililopokelewa ni kwamba (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) baada ya kuzika alikuwa akisema:

“Muombeeni msamaha ndugu yenu na mumtakie uthabiti. Hakika hivi sasa ataulizwa.”[1]

Lau ingelikuwa kusoma kwenye kaburi ni jambo limewekwa katika Shari´ah na ni zuri basi Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) angeliamrisha ili Ummah wake walijue.

Vilevile hakuna asli ya kuwakusanya watu majumbani ili wasome Qur-aan kwa ajili ya ile roho ya maiti. Salaf (Radhiya Allaahu ´anhum) hawakuwa wakilifanya. Pindi muislamu anapofikwa na msiba kilichowekwa katika Shari´ah ni yeye kusubiri na kutarajia malipo kutoka kwa Allaah na aseme yale wanayosema wenye subira:

“Hakika sisi ni wa Allaah na Kwake ndiko tutarejea. Ee Allaah! Nilipe kwa msiba wangu na unipe kilicho bora zaidi kuliko hicho.”

Ama kukusanyika kwenye familia ya yule maiti na kusoma Qur-aan, kupeana chakula na mfano wa hayo ni Bid´ah.

[1] Abu Daawuud (3221).

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Majmuu´-ul-Fataawaa (17/218-219)
  • Imechapishwa: 01/09/2021