Ni ipi hukumu ya kifuniko kinachowekwa juu ya kitanda cha maiti ya mwanamke wakati wa mchakato wa mazishi?

Swali: Unasemaje juu ya sanduku linalowekwa juu ya machela ya maiti ya mwanamke wakati wa mchakato wa mazishi?

Jibu: Haina neno. Baadhi ya wanazuoni wanasema kuwa inapendeza kufanya hivo. Katika kitabu cha Hanaabilah “ar-Rawdhw al-Murbiy“ imekuja ifuatavyo:

“Ikiwa ni jeneza la mwanamke basi inapendeza kumfunika kwa sanduku. Kwanza kufanya hivo kunamstiri zaidi na isitoshe imepokelewa kwamba Faatwimah (Radhiya Allaahu ´anhaa) aliamrisha atengenezewe sanduku kama hilo. Kisha sanduku hiyo itafunikwa na shuka.”[1]

Vilevile imekuja katika kitabu cha Maalikiyyah ”Jawhar-ul-Ikliyl Sharh Mukhtaswar Khaliyl”:

“Wakati wa kumbeba na kipindi cha kumswalia maiti wa kike inapendeza kumfunika kwa sanduku ili asitirike vyema zaidi.”[2]

Pia imekuja katika kitabu cha Shaafi´iyyah ”al-Majmuu´ Sharh al-Muhadhdhab”:

“Wenzetu wamependekeza mwanamke afunikwe na sanduku ambalo litawekwa katika ile machela ya maiti ya mwanamke. Halafu atafunikwa kwa shuka ili watu wasiweze kumuona. Hivo pia ndivo alivosema mtunzi wa “al-Haawiy”.”

Mpaka alipofikia kusema:

“Wamejengea hoja kwa kisa cha jeneza la mama wa waumini Zaynab (Radhiya Allaahu ´anhaa).  al-Bayhaqiy amepokea kuwa Faatwimah (Radhiya Allaahu ´anhaa) aliacha anausia afanyiwe sanduku, wakatekeleza. Ikiwa jambo hilo limesihi basi yeye ni baada ya Zaynab kwa miaka mingi.”[3]

Katika kitabu cha ´Abdur-Rahmaan al-Jaaziyriy ”al-Fiqh ´alaa al-Madhaahib al-Arba´ah” kumenakiliwa maoni ya Hanafiyyah ambao wamesema:

“Inapendeza kufunika kitanda cha maiti ya mwanamke kama inavofunikwa kaburi yake wakati wa kumzika mpaka pale atakapowekwa kwenye mwanandani wake. Kwa sababu mwili mzima mzima wa mwanamke ni ´Awrah; kuanzia miguuni mwake mpaka kichwani mwake.”[4]

Hivi ndivo yanavosema madhehebu manne. Hoja yao ni kwamba kufanya hivo kunamsitiri vyema zaidi mwanamke. Hili ni jambo linalotambulika na kufanyiwa kazi Hijaaz. Hata hivyo inatosha kufunika nusu ya mwili wa mwanamke chini kidogo ya kiuno chake kwa sanduku na juu ya sanduku kukafungwa kitambaa kwenye ncha ya machela. Isitoshe kufanya hivo ni kwepesi kidogo kuliko sanduku kubwa.

[1] ar-Rawdhw al-Murbiy´ (1/348).

[2] Jawhar-ul-Ikliyl Sharh Mukhtaswar Khaliyl (1/111).

[3] al-Majmuu´ Sharh al-Muhadhdhab (5/221).

[4] al-Fiqh ´alaa al-Madhaahib al-Arba´ah (1/531).

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Majmuu´-ul-Fataawaa (17/175-176)
  • Imechapishwa: 23/05/2022