Imaam an-Nawawiy (Rahimahu Allaah) amesema:

عن ابن عباس رضي الله عنهما قَالَ: قَالَ رَسُول الله صلى الله عليه وسلم: (نِعْمَتَانِ مَغبونٌ فيهما كَثيرٌ مِنَ النَّاسِ: الصِّحَّةُ، وَالفَرَاغُ). رواه البخاري

97 – Ibn ´Abbaas (Radhiya Allaahu ´anhumaa) ameeleza kuwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Kuna neema mbili ambazo wameghafilika nazo watu wengi; uzima na wakati.”

Ameipokea al-Bukhaariy.

Mtu anapokuwa na wakati na afya njema hupoteza sana neema mbili hizi. Wakati wetu mwingi unapotea pasina faida ilihali tuna afya njema na nafasi. Pamoja na hivyo vinatupotea sana. Ughafilikaji huu hatuuoni hapa duniani bali huzinduka na kuuona pale mtu anapofikwa na mauti na siku ya Qiyaamah. Dalili ya hilo ni pale Allaah (Ta´ala) aliposema:

حَتَّىٰ إِذَا جَاءَ أَحَدَهُمُ الْمَوْتُ قَالَ رَبِّ ارْجِعُونِ لَعَلِّي أَعْمَلُ صَالِحًا فِيمَا تَرَكْتُ

“Mpaka itakapomfikia mmoja wao mauti, atasema: “Mola wangu! Nirejeshe ili nikatende mema katika yale niliyoyaacha.”[1]

وَأَنفِقُوا مِن مَّا رَزَقْنَاكُم مِّن قَبْلِ أَن يَأْتِيَ أَحَدَكُمُ الْمَوْتُ فَيَقُولَ رَبِّ لَوْلَا أَخَّرْتَنِي إِلَىٰ أَجَلٍ قَرِيبٍ فَأَصَّدَّقَ وَأَكُن مِّنَ الصَّالِحِينَ

“Toeni baadhi ya vile Tulivyokuruzukuni kabla mmoja wenu hayajamfikia mauti akasema ´Mola wangu lau Ungelichelewesha mpaka muda wa karibu hivi, nikatoa swadaqah na nikawa miongoni mwa waja wema`.”[2]

Allaah (´Azza wa Jall) amesema:

وَلَن يُؤَخِّرَ اللَّـهُ نَفْسًا إِذَا جَاءَ أَجَلُهَا ۚ وَاللَّـهُ خَبِيرٌ بِمَا تَعْمَلُونَ

“Allaah haicheleweshi kamwe nafsi yeyote unapofika wakati wake; na Allaah ni Mjuzi wa khabari mzitendazo.”[3]

Uhakika ni kwamba wakati huu hutupotea bure tu. Sisi hatunufaiki nao na hatuwanufaishi wengine nao. Hatujutii hili isipokuwa pale tunapofikwa na mauti. Hapa ndipo binadamu atatamani angalau kupewa dakika moja tu ili aweze kuchuma, lakini hata hivyo hatopata hilo.

Isitoshe ni kwamba mtu anaweza asikose neema hizi mbili, ambayo ni ya wakati na afya kwa kujiwa na mauti, lakini neema hizi mbili anaweza kuzikosa kabla ya kufa. Anaweza kuuguwa maradhi ambayo hatoweza kusimama kwa yale aliyoamrishwa na Allaah. Anaweza kuumwa na akawa na dhiki kwenye kifua chake na akachoka. Vilevile anaweza kufanya kazi ili kujitatufia riziki yeye na familia yake mpaka akapitwa na mambo mengi ya ´ibaadah.

Kwa ajili hii inatakikana kwa mtu mwenye busara kutumia fursa ya uzima na nafasi kwa kumtii Allaah (´Azza wa Jall) kwa kiasi na anavyoweza. Ikiwa ni msomaji wa Qur-aan basi azidishe kusoma sana Qur-aan. Ikiwa hajui kusoma Qur-aan basi azidishe kumdhukuru kwa wingi Allaah (´Azza wa Jall). Ikiwa hawezi kuamrisha mema na kukataza maovu, awape na kuwadhamini kile anachoweza ndugu zake wawezao kufanya hiyo kazi. Kheri zote hizi zinatupita bure. Mtu mwenye akili ni yule anayeitumia fursa ya afya na ya wakati.

[1] 23:99-100

[2] 63:10

[3] 63:11

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Riyaadh-is-Swaalihiyn (02/66-67)
  • Imechapishwa: 24/10/2023