Swali: Nataraji utatoa nasaha za kidhahabu kuwapa baadhi ya vijana wenye msimamo wa dini ambao wanatumia muda mwingi kwenye intaneti na Allaah akujaze kheri.

Jibu: Ni jambo linalotambulika kuwa intaneti ina kheri na shari. Yule mwenye kutaka mambo mazuri atayapata. Ndani yake kuna elimu mbalimbali za Kishari´ah, elimu za kilugha, elimu za kisayansi na nyenginezo. Vilevile kuna shari nyingi. Nimefikiwa na khabari kwamba ina khatari zaidi kuliko hizi chaneli za satelaiti.

Kwa hivyo nasaha zangu kwa ndugu zangu – haihusiani na intaneti wala chaneli za satelaiti – ni kwamba wamche Allaah juu ya nafsi zao. Watambue kuwa hawakuumbwa kwa ajili ya jambo hili. Wameumbwa ili wamwabudu Allaah (´Azza wa Jall) na kwamba wakijishusha katika yale yanayofanana na wanyama ambapo watafuata matamanio na shahawa zao basi wamekhasirika duniani na Aakhirah. Kwa hivyo ni lazima kwa ndugu zangu waislamu waihifadhi dini yao na wachunge wakati wao na wasipoteze umri huu wenye thamani ya hali ya juu.

Naapa kwa Allaah kwamba dakika moja ni tukufu zaidi kuliko dirhamu elfu. Mnaonaje lau kifo kitamfikia mtu na akaambiwa atoe vyote alivyonavyo duniani ili acheleweshwe dakika moja tu basi ataitikia. Kwa ajili hii Allaah (´Azza wa Jall) amesema:

حَتَّىٰ إِذَا جَاءَ أَحَدَهُمُ الْمَوْتُ قَالَ رَبِّ ارْجِعُونِ لَعَلِّي أَعْمَلُ صَالِحًا فِيمَا تَرَكْتُ ۚ كَلَّا ۚ إِنَّهَا كَلِمَةٌ هُوَ قَائِلُهَا ۖ وَمِن وَرَائِهِم بَرْزَخٌ إِلَىٰ يَوْمِ يُبْعَثُونَ

“Mpaka kitakapomfikia mmoja wao kifo atasema: “Mola wangu! Nirejeshe ili nikatende mema katika yale niliyoyaacha.” [Ataambiwa] Sivyo kabisa! Hakika hilo ni neno alisemaye yeye tu na nyuma yao kuna kizuizi mpaka siku watakayofufuliwa.”[1]

Namuomba Allaah atupe sote mwisho mwema. Kwa ajili hii imekuja katika Hadiyth isemayo:

“Hakuna maiti yeyote anayekufa isipokuwa hujuta. Akiwa ni mwema basi anajuta ni kwa nini hakujizidishia na akiwa ni muovu anajuta ni kwa nini alifanya vibaya.”

Ndugu! Chunga umri wako! Ninaapa kwa Allaah kwamba ni wenye thamani zaidi kuliko dhahabu na fedha. Ikiwa mtu anachunga asipoteze dirhamu moja tu, ni vipi basi atapoteza umri wake ambao ndani yake ndio ima kuna kufaulu au kuangamia? Ee Allaah! Tunakuomba tuwe miongoni mwa wenye kufaulu. Ee Allaah! Tunakuomba tuwe miongoni mwa wenye kufaulu. Ee Allaah! Tunakuomba tuwe miongoni mwa wenye kufaulu, ee Mola wa walimwengu.

[1] 23:99-100

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: al-Liqaa´ ash-Shahriy (72) http://binothaimeen.net/content/1655
  • Imechapishwa: 16/08/2020