Kubadilisha maeneo baada ya swalah ya faradhi

3173- Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Umefanya vizuri Ibn-ul-Khattwaab.”

Ameipokea Ahmad: Muhammad bin Ja´far ametuhadithia: Shu´bah ametuhadithia, kutoka kwa al-Azraq bin Qays, kutoka kwa ´Abdullaah bin Rabaah, kutoka kwa mmoja katika Mswahabah wa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Baada ya Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kumaliza kuswali ´Aswr, alisimama bwana mmoja kuswali. Wakati ´Umar alipomuona akachukua nguo au kanzu yake na akasema: “Keti chini. Hakika si vyenginevyo kilichowaangamiza watu wa Kitabu ni kwamba hakukuwa na kipambanuzi kati ya swalah zao.” Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akasema: “Umefanya vizuri Ibn-ul-Khattwaab.”

Hadiyth inajulisha kuwa ni lazima kupambanua kati ya swalah ya faradhi na swalah ya sunnah. Kupambanua kunakuwa ima kwa maneno au kubadilisha maeneo, jambo ambalo kuna Hadiyth Swahiyh nyingi juu ya hilo… Yale yanayofanywa hii leo katika baadhi ya miji baada kumaliza kuswali swalah ya faradhi ambapo watu wanabadilisha maeneo yao kwa ajili ya kuswali swalah ya sunnah, ni katika kule kubadilisha maeneo kulikotajwa. Salaf pia walifanya hivo. Ibn Abiy Shaybah alisema:

“Niliswali swalah ya ijumaa pamoja na ´Aaswim. Nilipomaliza swalah yangu alinishika mkono wangu na tukabadilishana maeneo.”

Cheni ya wapokezi wake ni Swahiyh. Amepokea mfano wake kutoka kwa Abu Mijlaz na Swafwaan bin Muhriz.

  • Mhusika: Imaam Muhammad Naaswir-ud-Diyn al-Albaaniy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Silsilat-ul-Ahaadiyth as-Swahiyhah (7/1/522)
  • Imechapishwa: 16/08/2020