Namna mbili ya kunuia swalah za faradhi

Swalah za faradhi ni tano: Fajr, Dhuhr, ´Aswr, Maghrib na ´Ishaa. Unapokuja msikitini wakati wa alfajiri ni swalah ipi unayotaka kuswali? Je, wataka kuswali Maghrib? Hapana. Bali ni Fajr. Umekuja na kusema “Allaahu Akbar” na wewe umenuia, lakini kwenye fahamu zako imekupotea ni swalah ipi unayotaka kuswali. Hili ni jambo linalotokea mara nyingi na khaswa pale ambapo mtu ana haraka na kuogopa asipitwe na Rak’ah. Kwa mfano mtu anakuja na kusema “Allaahu Akbar”, lakini hukuhudhurisha kwenye fahamu zako ya kwamba unataka kuswali Fajr. Tunasema kuwa hakuna haja. Kuja wakati wa swalah hii ni dalili tosha ya kwamba umenuia kuswali swalah hii. Ndio maana lau yeyote atakuuliza ni swalah ipi unataka kuswali; Dhuhr, ´Aswr, Maghrib au ´Ishaa? Jibu lako utasema unakusudia kuswali Fajr. Hivyo hakuna haja ya kunuia kuwa ni Fajr.

Ni kweli lau utaweka katika fahamu yako kuwa ni Fajr ni ukamilifu zaidi. Lakini wakati mwingine mtu inampotea akilini mwake. Tunasema kinachoilenga ni wakati.

Kwa hivyo faradhi inanuiwa kwa njia mbili:

1 – Kuilenga kwa moyo kwa mfano kunuia Dhuhr. Hili liko wazi.

2 – Wakati. Maadamu unaswali swalah kwa wakati huu, basi hukulenga nyingine isipokuwa ilio katika wakati huu.

Hii njia ya pili inakuwa kwa swalah yenye kuswaliwa kwa wakati wake. Lakini kwa mfano tukichukulia ya kwamba mtu anatakiwa kukidhi swalah nyingi, kwa mfano amepitikiwa na usingizi siku nzima na hivyo Dhuhr, ´Aswr na Maghrib zikawa zimempita, katika hali hii akitaka kuziswali ni lazima anuie kwa kuwa wakati wake umepita.

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Riyaadh-is-Swaalihiyn (01/378-379)
  • Imechapishwa: 24/05/2023