52. Tofauti kati ya mfumo na chombo

Kwa sababu tu tumethibitisha kuwa njia za ulinganizi zinatakiwa ziafikiane na Qur-aan na Sunnah, haina maana kuwa tunakataa vyombo vya kisasa na vifaa vilivyotengenezwa katika nyanja mbalimbali. Muda wa kuwa vyombo hivyo vinaruhusiwa na Shari´ah, basi hapana vibaya kuvitumia wakati wa kulingania. Kwani hakika vyombo hivyo viko kwa ajili ya kufikisha ulinganizi; muda wa kuwa vyenyewe kama vyenyewe havijakataliwa, basi hapana vibaya kuvitumia.

Kwa mfano mikrofoni iko kwa ajili ya kufikisha sauti ambayo yenyewe kama yenyewe ni njia iliyowekwa katika Shari´ah katika kulingania kwa Allaah. ´Aaishah (Radhiya Allaahu ´anhaa) amesema:

“Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alimwamrisha Abu Bakrawaswalishe watu wakati alipoumwa, ambapo akawa anawaswalisha. Wakati mmoja Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akajihisi nguvu akatoka wakati ambapo Abu Bakr alikuwa anawaswalisha watu. Wakati Abu Bakr alipomuona akarudi nyuma, akamwashiria abaki mahali pake. Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akakaa usawa pambizoni mwa Abu Bakr. Abu Bakr akawa anaswali kwa kumfuata Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na watu wanaswali kwa kumfuata Abu Bakr.”

Salaf pia walifanya hivo.

Mfano mwingine ni kaseti. Yenyewe kama yenyewe sio mfumo na njia ya kulingania. Kuna manufaa gani ya kaseti iliotupu? Ni chombo kinachofikisha au kinachohifadhi mada iliyorekodiwa. Mfumo na njia ni ile mada iliyorekodiwa ambayo ni njia iliyowekwa katika Shari´ah. Kuhusu kaseti yenyewe kama yenyewe sio mfumo na njia ya ulinganizi, isipokuwa ile kheri inayowekwa ndani yake.

Vivyo hivyo mashine za faksi. Zinaweza kufananishwa na wale wajumbe waliokuwa wakipeleka barua za Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kwa wafalme, viongozi na kadhalika. Kwa hivyo ikiwa mfumo wa ulinganizi unafikishwa kwa chombo kinachoruhusiwa, tutakiruhusu, na ikiwa kiko na haramu, tutakiharamisha.

  • Mhusika: Shaykh ´Abdus-Salaam bin Barjas Aal ´Abdil-Kariym
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: al-Hujaj al-Qawiyyah ´alaa anna Wasaa-il-ad-Da´wah Tawqiyfiyyah, uk. 72-73
  • Imechapishwa: 24/05/2023