Mwenye kuacha swalah hahijiwi wala hatolewi swadaqah yoyote

Swali: Unasemaje juu ya ambaye anatoa zawadi ya matendo mema kukiwemo kisomo cha Qur-aan, hijjah na ´umrah kumpa mtu ambaye amekufa pasina kuswali na mara nyingi mtu huyu anakuwa mjinga na si msomi?

Jibu: Mwenye kuacha swalah hahijiwi na wala hatolewi swadaqah. Kwa sababu ni kafiri kwa mujibu wa maoni sahihi zaidi ya wanazuoni. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Baina ya mtu na shirki na ukafiri ni kuacha swalah.”

Ameipokea Muslim katika “as-Swahiyh” yake.

Vilevile amesema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Ahadi iliopo kati yetu sisi na wao [makafiri] ni swalah. Hivyo basi, yule mwenye kuiacha amekufuru.”

Ameipokea Imaam Ahmad na watunzi wa as-Sunan kwa cheni ya wapokezi Swahiyh.

Kusoma juu ya wengine ni kitu ambacho hakikuwekwa katika Shari´ah. Ni mamoja anasomewa ambaye yukohai au maiti. Hakuna dalili juu ya hilo. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Yeyote atakayefanya kitendo kisichoafikiana na amri yetu basi atarudishiwa mwenyewe.”

Ameipokea Muslim katika “as-Swahiyh” yake. Mashaykh wawili, ambao ni al-Bukhaariy na Muslim, wamepokea kwa tamko lisemalo:

“Yeyote atakayezua katika amri yetu hii yale yasiyokuwemo atarudishiwa mwenyewe.”

 Kutokana na tunavojua haikuthibiti kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) wala Maswahabah (Radhiya Allaahu ´anhum) kwamba walisoma Qur-aan na kumpa thawabu zake aliyehai au maiti.

  • Mhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Majmuu´-ul-Fataawaa (10/251)
  • Imechapishwa: 10/09/2021