Swali: Ni ipi hukumu ya ambaye anakufa ilihali haswali pamoja na kuzingatia kwamba wazazi wake wawili ni waislamu? Mtu achukue msimamo gani inapokuja katika kumuosha, kumvika sanda, kumswalia, kumzika, kumuombea du´aa na kumtakia rehema?

Jibu: Anayekufa katika wale watu ambao ´ibaadah zinawawajibikia ilihali haswali ni kafiri. Hivyo hatooshwa, hatoswaliwa, hatozikwa kwenye makaburi ya waislamu na jamaa zake hawatomrithi. Bali mali yake itaenda katika wizara ya fedha. Hivi ni kwa mujibu wa maoni sahihi zaidi ya wanachuoni. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema katika Hadiyth Swahiyh:

“Baina ya mtu na shirki na ukafiri ni kuacha swalah.”

Ameipokea Imaam Muslim katika “as-Swahiyh” yake.

Vilevile amesema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Ahadi iliopo kati yetu sisi na wao [makafiri] ni swalah. Hivyo basi, yule mwenye kuiacha amekufuru.”

Ameipokea Imaam Ahmad na watunzi wa as-Sunan kwa cheni ya wapokezi Swahiyh kupitia kwa Buraydah (Radhiya Allaahu ´anh). ´Abdullaah bin Shaqiyq, ambaye ni mwanafunzi mtukufu wa Maswahabah (Rahimahu Allaah), amesema:

“Maswahabah wa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) hakuna kitu katika matendo walikuwa wakionelea kukiacha ni kufuru isipokuwa swalah.”

Zipo Hadiyth na mapokezi mengi yenye maana kama hii. Hukumu hii ni juu ya yule mwenye kuiacha kwa uvivu na hakupinga kwamba ni wajibu. Kuhusu ambaye anapinga uwajibu wake ni kafiri na mwenye kuritadi nje ya Uislamu kwa maafikiano ya wanazuoni wote.

  • Mhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Majmuu´-ul-Fataawaa (10/250)
  • Imechapishwa: 10/09/2021