Mwanamke kutoka kulingania kwa mtazamo wa Ibn Baaz

Swali: Je, inafaa kwa mwanamke wa kiislamu kutoka kwa wingi nje ya nyumba kwa ajili ya kulingania katika dini ya Allaah (Ta´ala)?

Jibu: Hiki ni kitendo chema. Mwanamke kutoka kwa ajili ya kulingania ni kitendo chema. Kuhusu maneno Yake (Ta´ala):

وَقَرْنَ فِي بُيُوتِكُنَّ

“Tulizaneni majumbani mwenu.” (33:33)

Amri ya kutulizana nyumbani ni pale ambapo hakuna haja. Lakini kukiweko haja, kama mfano wa kutoka kwa ajili ya kuwapa mawaidha na kuwakumbusha wanawake wenziwe au akatoka kwa ajili ya kushuhudia swalah pamoja na wanamme kwa ajili ya manufaa aliyoyaona sambamba na hilo akavaa Hijaab na akajisitiri. Wanawake wa Maswahabah walitoka wakati wa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kwa ajili ya kuswali pamoja na Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) msikitini mwake pamoja na kuvaa Hijaab na kujisitiri.

Vivyo hivyo inafaa kwake kutoka kwa ajili ya kuwatembelea wazazi wake au jamaa zake pamoja na kuvaa Hijaab na kujisitiri, kuwatembelea wagonjwa, kuwapa pole waliofikwa na msiba, kwa ajili ya kulingania kwa Allaah au mfano wa mambo hayo miongoni mwa malengo mazuri. Lakini sambamba na hilo wachunge yale aliyoamrisha Allaah katika Hijaab, kujisitiri, kutoonyesha mapambo na kutofanya yale mambo yanayosababisha fitina.

Wanawake wanayo haja ya kulingania kama ambavo wanamme pia wanayo haja ya kulingania na kila mmoja anahitaji ulinganizi. Endapo mwanamke huyo atawanasihi na kuwapa mawaidha wanamme pia ni sawa.  Tumekwishatangulia kutaja kwamba sauti ya mwanamke sio uchi. Sauti yake wakati wa kulingania katika dini ya Allaah, kuelekeza katika mambo ya kheri na kukataza maovu sio uchi. Uchi ni pale ambapo atajidekeza na kujilainisha, kama tulivyotangulia kutaja.

  • Mhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: https://binbaz.org.sa/fatwas/4243/حكم-خروج-المراة-للدعوة-الى-الله-تعالى
  • Imechapishwa: 11/06/2022