Msimamo wa muislamu juu ya Mitume waliyotangulia

Ni lazima kwetu kumfuata Mtume wa mwisho Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kwa kuwa yeye ndiye ambaye tumefaradhishiwa kumfuata. Allaah (Ta´ala) amesema:

قُلْ يَا أَيُّهَا النَّاسُ إِنِّي رَسُولُ اللَّـهِ إِلَيْكُمْ جَمِيعًا الَّذِي لَهُ مُلْكُ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضِ ۖ لَا إِلَـٰهَ إِلَّا هُوَ يُحْيِي وَيُمِيتُ ۖ فَآمِنُوا بِاللَّـهِ وَرَسُولِهِ النَّبِيِّ الْأُمِّيِّ الَّذِي يُؤْمِنُ بِاللَّـهِ وَكَلِمَاتِهِ وَاتَّبِعُوهُ لَعَلَّكُمْ تَهْتَدُونَ 

“Enyi watu! Hakika mimi ni Mtume wa Allaah kwenu nyinyi nyote wa [Yule] ambaye pekee anao ufalme wa mbingu na ardhi! Hapana mungu wa haki ila Yeye – Anahuisha na anafisha. Basi mwaminini Allaah na Mtume Wake, ambaye hajui kuandika wala kusoma, ambaye anamwamini Allaah na maneno Yake na mfuateni ili mpate kuongoka.” (07:158)

Allaah ametuamrisha kumfuata. Allaah (Ta´ala) amesema tena:

قُلْ إِن كُنتُمْ تُحِبُّونَ اللَّـهَ فَاتَّبِعُونِي يُحْبِبْكُمُ اللَّـهُ

“Sema:“Mkiwa mnampenda Allaah, basi nifuateni atakupendeni Allaah.” (03:31)

Ama kuhusu Mitume wengine, sisi tunawafuata pale ambapo Shari´ah yetu itatuamrisha kuwafuata. Kwa mfano maneno yake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Swalah bora ni ya ndugu yangu Daawuud. Alikuwa akilala nusu ya usiku na akisimama theluthi na akilala sudusi yake. Swawm bora ni ya ndugu yangu Daawuud. Alikuwa akifunga siku moja na kula ya kufuata.”[1]

Haya ni maelezo juu ya ´ibaadah za Daawuud na kusimama kwake usiku na swawm yake. Tumeelezwa ili na sisi tuweze kumfuata.

Ama ikiwa Shari´ah yetu haikutuamrisha kumfuata, wanachuoni (Rahimahumu Allaah) wametofautiana  kama Shari´ah ya waliokuwa kabla yetu ni Shari´ah yetu vilevile midhali hakukuja kitu katika Shari´ah yetu kinachoenda kinyume nacho au sio Shari´ah yetu mpaka pale Shari´ah yetu itapotuamrisha kuifuata? Sahihi ni kwamba Shari´ah ya waliokuwa kabla yetu ni Shari´ah yetu vilevile ikiwa hakukuja kitu katika Shari´ah yetu kinachoenda kinyume nayo. Kwa sababu Allaah (Ta´ala) baada ya kuwataja Manabii na Mitume alimwambia Mtume wetu (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

أُولَـٰئِكَ الَّذِينَ هَدَى اللَّـهُ ۖ فَبِهُدَاهُمُ اقْتَدِهْ

“Hao ndio ambao Allaah amewaongoa. Hivyo basi fuata kama kigezo mwongozo wao.” (06:90)

Hivyo Allaah akamuamrisha Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) afuate uongofu wa waliyotangulia. Allaah (Ta´ala) amesema pia:

لَقَدْ كَانَ فِي قَصَصِهِمْ عِبْرَةٌ لِّأُولِي الْأَلْبَابِ

“Kwa hakika katika visa vyao kuna mazingatiokwa wenye akili.” (12:111)

Aayah hii iko mwishoni wa Suurah Yuusuf ambapo ndani yake Allaah (Ta´ala) ametaja kisa chao [Mitume] kirefu ili tuweze kuzingatia yaliyomo.

[1]al-Bukhaariy (1131).

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Riyaadh-is-Swaalihiyn (01/452-453)
  • Imechapishwa: 19/06/2023