54 – Muhammad bin Yahya bin Abiy Haatim ametuhadithia: Yaziyd bin Haaruun ametuhadithia: Sufyaan bin Husayn ametukhabarisha, kutoka kwa al-Hasan, ambaye amesema:

”Wakati Ibn ´Umar alipokuwa anakula chakula cha mchana na chakula cha jioni, alikuwa akiwaita mayatima waliokuwa pambizoni mwake. Siku alipokuwa anataka kula chakula cha mchana, alimtumia yatima mjumbe, lakini hakumpata. Alikuwa na supu ya maziwa aliyokuwa anakunywa baada ya chakula chake cha mchana. Yatima yule akaja baada ya kwamba wamemaliza kula. Akampa supu ya maziwa aliokuwa nayo mkononi mwake na akasema: ”Sioni kama umetendewa haki.”

55 – Muhammad bin Yahyaa ametuhadithia: Muhammad bin Saabiq ametuhadithia: Maalik bin Mighwal amesema:

”Nilisikia kuwa walimpikia chakula – bi maana Ibn ´Umar – ambapo wakamletea nacho pamoja na mkate. Alipotaka kuwagawia nacho masikini, wakaondoka naye. Ndipo akasema: ”Mmenizuia kulisha na nataka kukitupa kwenye takataka. Naapa kwa Allaah! Sintokionja hii leo!”

56 – Muhammad bin Yahyaa amenihadithia: ´Attaab bin Ziyaad ametuhadithia: ´Abdullaah ametuhadithia: al-Mufadhdhwal bin Laahiq ametuhadithia, kutoka kwa Abu Bakr bin Hafsw, ambaye amesema:

”Ibn ´Umar alikuwa hawazuii walio na ugonjwa wa ukoma, ugonjwa wa vitiligo wala watu waliopewa mtihani kati ya Makkah na Madiynah kutokana na chakula chake kuketi na kula pamoja naye. Walikuwa wakiketi naye kwenye meza ya chakula. Siku moja wakati alipokuwa amekaa kwenye meza yake ya chakula, walikuja watumwa wake wawili wa Madiynah. Wakawakaribisha na kuwafanyia nafasi. ´Abdullaah akacheka, ambapo wale watumwa wawili wakachukulia vibaya na kusema: ”Unacheka, ee Abu ´Abdir-Rahmaan – Allaah akufurahishe. Ni kipi kilichokufanya kucheka?” Akasema: ”Nashangazwa na watu hawa wana wangu ambao midomo yao inatoka damu kutokana na njaa; wananyanyaswa na kuudhiwa nao. Endapo mmoja wao angeliweza kuchukua nafasi ya watu wawili, basi angelifanya hivo kwa ajili ya kuwaudhi na kuwanyanyasa. Lakini mlipokuja nyinyi wawili, wamekuwekeeni chakula, wakawafanyia nafasi na kukukaribisheni. Wanampikia chakula asiyekitaka na wanamnyima nacho anayekitaka.”  

57 – Muhammad bin Yahyaa bin Abiy Haatim amenihadithia: Bakr bin Khaddaash ametuhadithia: Maalik bin Mighwal ametuhadithia, kutoka kwa Naafiy´, ambaye amesema:

”Ibn ´Umar aliletewa uji wa ngano akasema: ”Ni kitu gani hiki?” Wakasema: ”Ni kizuri kwa kusaga chakula.” Ndipo akasema: ”Huletewa chakula fulani na fulani, lakini sili kushiba.”

58 – Nimehadithiwa kutoka kwa ´Abdul-´Aziyz bin Muhammad, kutoka kwa ´Ubaydullaah bin ´Umar, kutoka kwa Naafiy´, kutoka kwa Ibn ´Umar, ambaye amesema:

”Sijawahi kushiba tangu niliposilimu.”

  • Mhusika: Imaam Abu Bakr ´Abdullaah bin Muhammad bin Abiyd-Dunyaa
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Kitaab-ul-Juu´, uk. 59-61
  • Imechapishwa: 19/06/2023