Madhehebu ya Ahl-us-Sunnah inapokuja katika Sifa za Allaah (Ta´ala) ni kuthibitisha Sifa za kidhati; kama mfano wa kusikia na kuona, na kuthibitisha Sifa za kimatendo; kama mfano wa kuridhia, kupenda, kuchukia, kufanya uadui [kwa wale wanaomfanya Allaah uadui], mapenzi, maneno na nyinginezo ambazo zimethibiti katika Qur-aan na Sunnah. Zinathibitishwa kama inavyolingana na Utukufu na Ukubwa wa Allaah na kuepuka Ta´wiyl ambayo inazitoa katika uhakika wake inayolingana na Utukufu wa Allaah (Ta´ala). Kwa msemo mwingine wanazithibitisha bila ya kuzipotosha, kuzikanusha, kuzitilia namna na kuzipigia mifano.

Madhehebu ya Mu´awwilah inapokuja katika Sifa za Allaah (Ta´ala) za kidhati na za kimatendo kama mfano wa Jahmiyyah na Mu´tazilah. Watu hawa wanakanusha kila kile ambacho Allaah amejisifia Mwenyewe katika Sifa za kidhati na za kimatendo. Wanasema kuwa ni kitu kilichoumbwa, kilicho na kikomo na kilichotengana na Allaah na hakufungamana na chochote katika hayo. Utata wao wanasema lau tutamsifu kwa Sifa za kimatendo na kisifa basi atakuwa na viungo ilihali Allaah ametakasika na hayo.

Wanaraddiwa kwa kujibiwa ya kuwa hizi ni Sifa za kimatendo na sio Sifa za viungo. Kuita kuwa ni Sifa za viungo ni istilahi yenu nyinyi. Kujengea juu ya hili mnakanusha yale ambayo Allaah amejisifu kwayo katika Kitabu Chake na kupitia ulimi wa Mtume Wake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam).

Madhehebu ya Kullaabiyyah na Ashaa´irah inapokuja katika Sifa za kimatendo. Kwa mujibu wao asli ni kuwa Allaah hasifiwi kwa kitu chenye kufungamana na matakwa na uwezo Wake. Kwa msemo mwingine wanakanusha Sifa za kimatendo. Wanaonelea kuwa hakuna wakati ambapo anakuwa ni mwenye kuridhia na wakati mwingine hawi hivo, vivyo hivyo kukasirika, hazungumzi pale anapotaka na wala hacheki pale anapotaka. Mambo ya kimatendo yote haya ni yenye kulazimiana na dhati Yake ya tangu hapo kale ya milele. Utata wao wanasema lau yangelikuwa ni yenye kujitokeza wakati fulani na wakati mwingine hasifiki nayo, basi angelikuwa ni sehemu ya matukio. Kwa ibara nyingine wanasema kuwa Sifa za kimatendo ni zenye kujitokeza na ni Sifa zilizosimama katika dhati. Wanaonelea kuwa ni za tangu hapo kale na kitu cha tangu hapo kale sio sehemu ya kujitokeza.

Wanaraddiwa kwa kuambiwa ni Sifa za kimatendo na wala haziitwi kuwa ni matukio. Kama jinsi Sifa za dhati mmeita kuwa ni Sifa vivyo hivyo iteni Sifa za kimatendo kuwa ni Sifa na wala msiite kuwa ni matukio.

  • Mhusika: ´Allaamah ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah ar-Raajhiy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: al-Hidaayah ar-Rabbaaniyyah fiy Sharh al-´Aqiydah at-Twahaawiyyah (02/745-747)
  • Imechapishwa: 18/05/2020