Imaam an-Nawawiy (Rahimahu Allaah) amesema:

عن ابن مسعود رضي الله عنه قَالَ: قَالَ النَّبيّ صلى الله عليه وسلم: (الجَنَّةُ أَقْرَبُ إِلَى أَحَدِكُمْ مِنْ شِرَاكِ نَعْلِهِ، وَالنَّارُ مِثلُ ذلِكَ). رواه البخاري

105 – Ibn Mas´uud (Radhiya Allaahu ´anh) ameelezakuwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Pepo iko karibu zaidi na mmoja wenu kuliko kamba za viatu vyake. Na Moto ni vivyo hivyo.”

al-Bukhaariy

Huenda mtu vilevile akatamka neno baya asilolipa uzito ambalo likamkasirisha Allaah na ikawa ni sababu ya kumwingiza Motoni. Ni maneno mangapi mtu huzungumza pasina kujali na ikawa ni sababu ya kumwingiza Motoni. Tunamuomba Allaah afya.

Huoni kisa cha wanafiki ambao walikuwa pamoja na Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) katika vita vya Tabuuk pindi walipokuwa wakizungumza kati yao. Wakasema “Hatujaona watu kama wasomaji wetu hawa! Wanakula sana, wanasema uongo sana na ni waoga wakati wa mapambano” wakimaanisha Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na Maswahabah zake[1]. Namna hii ndivyo wanafiki walivosema juu ya Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na Maswahabah zake. Lau utazingatia utaona kuwa hili linawagusa wanafiki mia kwa mia na sio waumini. Wanafiki ndio watu wenye kupupia zaidi kuishi, wenye kusema uongo zaidi na waoga zaidi wakati wa mapambano. Waliyosema yanawastahiki zaidi wanafiki hawa. Allaah (´Azza wa Jall) akasema:

وَلَئِن سَأَلْتَهُمْ لَيَقُولُنَّ إِنَّمَا كُنَّا نَخُوضُ وَنَلْعَبُ

“Ukiwauliza bila shaka watasema: “Hakika tulikuwa tunaporoja na tunacheza.”

Bi maana hakutukuwa tukikusudia kweli. Ilikuwa ni porojo tu na kucheza. Allaah (´Azza wa Jall) akasema:

قُلْ

”Sema.”

Bi maana “Ee Muhammad! Waambie:

أَبِاللَّـهِ وَآيَاتِهِ وَرَسُولِهِ كُنتُمْ تَسْتَهْزِئُونَ لَا تَعْتَذِرُوا قَدْ كَفَرْتُم بَعْدَ إِيمَانِكُمْ  إِن نَّعْفُ عَن طَائِفَةٍ مِّنكُمْ نُعَذِّبْ طَائِفَةً بِأَنَّهُمْ كَانُوا مُجْرِمِينَ

”Je, mlikuwa mnamfanyia istihizai Allaah na Aayah Zake na Mtume Wake? Msitoe udhuru. Hakika mmekwishakufuru baada ya kuamini kwenu. Tukilisamehe kundi miongoni mwenu, basi tutaliadhibu kundi jingine kwa kuwa sababu walikuwa wahalifu.” (09:65-66)

Allaah (´Azza wa Jall) akabainisha kuwa watu hawa wamekufuru baada ya kuamini kwao kwa sababu ya kufanya istihzai na Allaah, Aayah Zake na Mtume Wake.

Kwa hiyo inapaswa kwa mtu achunge yale anayozungumza na auhifadhi ulimi wake ili asije akatekeza na hiyo ikawa ni sababu ya kuangamia.

[1] Tazama “Tafsiyr-ul-Qur-aan al-´Adhwiym” ya Ibn Kathiyr (02/301-302) Suurat-ut-Tawbah Aayah ya 65:66

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Riyaadh-is-Swaalihiyn (02/100-102)
  • Imechapishwa: 01/01/2024