Swali: Nimesoma maneno ya Shaykh Yuusuf al-Qaradhwaawiy juu ya mambo yanayosababisha tofauti. Anasema kuwa kila kitu kinachosababisha tofauti inatakiwa kukiacha hata kama kinahusiana na ´Aqiydah. Anajengea juu ya kisa cha Muusa na Haaruun (Swalla Allaahu ´alayhimaa wa sallam) ya kwamba Haaruun aliacha kuwakemea wana wa israaiyl kuabudia kwao ndama kwa sababu:

إِنِّي خَشِيتُ أَن تَقُولَ فَرَّقْتَ بَيْنَ بَنِي إِسْرَائِيلَ وَلَمْ تَرْقُبْ قَوْلِي

“Hakika mimi niliogopa usije kusema “Umefarikisha kati ya wana wa Israaiyl na wala hukuchunga kauli yangu.”[1]

Ni ipi Radd yako juu ya maneno haya? Bwana huyu ana wafuasi na wengi wanaompenda. Ni miongoni mwa wale wanaochanganya sumu na asali. Nimelinganisha vitabu vyake yeye na al-Ghazaaliy na nikaona kuwa vitabu vyake vina shari zaidi kuliko vya al-Ghazaaliy.

Jibu: Ni marafiki. Sidhani kuwa haya ni maoni mapya. al-Ikhwaan al-Muslimuun wanarithishana maoni haya kizazi baada ya kingine. Nimetaja katika matukio mengi makutano yangu mimi na kiongozi wa al-Ikhwaan al-Muslimuun Iraaq. Huyu alikuwa khatwiyb mwenye ufaswaha. Kama walivyo makhatwiyb wengi wa al-Ikhwaan al-Muslimuun wanaweza kuathiri hadhira. Kuna bwana mmoja kwa jina Hasan at-Twaffiy alikuwa anafanya kazi kwenye maktabah ya chuo kikuu wakati nilipokuwa nafundisha hapo. Kumeshapita zaidi ya miaka thelathini. Bwana huyo alinialika mimi na baadhi ya ndugu zetu nyumbani kwake kula chakula cha jioni ambapo ilikuwa katika maeneo ya chuo kikuu. Alikuwa pamoja nasi Shaykh ´Umar al-Ashqar ambaye alikuwa amejiunga na al-Ikhwaan al-Muslimuun. Tulikuwa kwenye chumba kikubwa tumejaa pamoja na ndugu zetu. Nilikuwa kama kawaida yangu nimekaa karibu na mlango. Kila anapoingia mtu basi anakaa chini. Huyo Shaykh aliyetajwa akaingia ndani. Yeye mwenyewe anajizingatia kuwa ni Salafiy. Ana kitabu kuhusu swalah. Akaingia ndani, akatoa salamu na kuwapa mkono wote waliokuwa pale. Ni mara chache mmoja katika sisi anafanya hivo. Nikaona namna ambavyo uso wake umebadilika. Hatimaye akanijilia. Nikaona kuwa hakupendezwa namna ambavyo ndugu zetu wamenyoosha mkono peke yake. Nikamwambia kwamba sisi kwetu Shaam husema kuwa mtu ni mtukufu hata kama hakusimamiwa. Akapiga makofi. Hakuamini kusikia hivyo. Akaanza kusema mfano wa maneno:

”Hivi tunaishi katika aina mbalimbali za ukafiri kama chama cha Ba´th, wakanamungu… Ni lazima tuachane na mambo yanayotutofautisha.”

Huyu ni khatwiyb na nina uzoefu kwamba ni nadra sana kukuta makhatwiyb wana sifa nyingi nzuri ikiwa ni pamoja na elimu na mjuzi mwenye kujua kufanya mjadala. Khawiyb anatoa khutbah, lakini hajadili. Akaanza ufaswaha wake kiasi cha kwamba wale watu wadhaifu wakaathirika na maneno yake. Nikamwambia kwamba maneno kwamba tuachane na mambo yenye tofauti yana ukhatari mkubwa. Kama unavyojua mambo ya tofauti sio katika mambo ya tanzu peke yake; yapo hata katika mambo ya misingi na katika Tawhiyd yenyewe. Nikamweleza kuwa kwetu Dameski kuna bwana mmoja anaitwa Shaykh Muhammad al-Maghribiy ambaye ni Shaykh wa mrengo wa Shaadhiliyyah. Ameandika kitabu chenye anwani ”Laa ilaaha illa Allaah”. Unapokisoma utaona namna anavyofasiri shahaadah kwa tafsiri ya Tawhiyd-ur-Rubuubiyyah – hapana mola isipokuwa Allaah. Nikamwambia kwamba tofauti ipo mpaka katika shahaadah. Unaposema kwamba tuachane na mambo yote yenye tofauti hiyo maana yake ni kwamba tusisome Tawhiyd. Akasema:

”Ndio! Turidhike na kutamka kwao hapana mungu wa haki isipokuwa Allaah.”

Hapo ndipo nilipokuwa napataka. Unataka kupambana na wakomunisti, chama cha Ba´th, wakanamungu na wengine kwa watu hawa wanaotamka shahaadah? Sijui hata kama wanaifahamu kama walivyoifahamu washirikina. Washirikina waliifahamu lakini wakaikufuru, ama watu hawa ni wajinga na wakaamin imani ya upofu. Kwa hiyo hili sio jambo geni kabisa.

[1] 20:94

  • Mhusika: Imaam Muhammad Naaswir-ud-Diyn al-Albaaniy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Silsilat-ul-Hudaa wan-Nuur (930) Tarehe: 1417-04-09/1996-08-24
  • Imechapishwa: 14/11/2022