Swali: Mimi naumwa maradhi yanayoitwa sinus ambayo yananifanya kushindwa kula nisipotumia dawa inayoitwa X.  Ninachotaka kusema ni kuwa mwaka jana katika mwezi wa swawm nilifunga mchana. Ilipofika wakati wa kufungua sikuweza kula hata kidogo kwa sababu ya kutotumia dawa hiyo ambayo inafungua njia za hewa na kumfanyia wepesi mtu kula kwa raha. Vilevile mwaka jana sikuweza kufunga kwa sababu ya maradhi hayo. Mimi namuogopa Allaah Mtukufu na sitaki kumuasi kwa chochote. Je, inafaa kwangu kutumia dawa hiyo takriban nusu saa kabla ya kufika wakati wa kukata swawm? Dawa hiyo ni ya tone inayowekwa puani. Nisipoitumia siwezi kufunga. Nikisubiri na kuitumia wakati wa kufungua ndio nikaweka puani, basi nitasubiri muda wa takriban nusu saa ndio nitaweza kula. Kutokana na ninavojua ni wajibu kuharakisha kukata swawm. Unaninasihi nini? Je, naweza kuitumia dawa hiyo ya tone puani takriban nusu saa kabla ya kufika wakati wa kufungua kwa sababu nimelazimika kufanya hivo?

Jibu: Haifai kwako kufanya hivo. Unatakiwa kuchelewesha futari mpaka ukamilishe funga yako. Ukikamilisha swawm yako ndio unaweza kuitumia. Kwa sababu Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amekhabarisha kuwa pua ni njia inayoweza kupitishwa kitu na ndio maana akasema:

“Fanya kishindo katika kupalizia isipokuwa unapokuwa umefunga.”

Pua ni njia inaweza kupitishwa maji na matone. Chelewesha kutumia dawa hiyo ya tone mpaka kuzame jua. Isipokuwa ikiwa ni tone dogo lisiloweza kupanda wala kushuka tumboni. Kwa maana nyingine linaishilia puani peke yake na halipandi kwenye ubongo wala halishuki kooni, kitu ambacho hakiwezekani. Dawa za tone zinakuwa na nguvu. Kwa kufupisha ni kwamba muda wa kuwa lina ushawishi kwenye ubongo au linashuka, basi icheleweshe mpaka jua lizame hata kama utachelewa.

Mwendaji kipindi: Lakini amesema kuwa itampeleka kuchelewa futari kwa nusu saa?

Ibn Baaz: Haidhuru hata kama atachelewa kwa saa moja.

Mwendaji kipindi: Kwa hiyo ndugu yetu afunge na watakapoadhini Maghrib ndipo itafaa kwake kutumia dawa ya tone na baada ya nusu saa ndio ale futari yake?

Ibn Baaz: Ndio.

  • Mhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: https://binbaz.org.sa/fatwas/9671/حكم-تعاطي-المريض-دواء-قبل-الافطار-في-رمضان
  • Imechapishwa: 26/03/2023