Inajuzu kupangusa juu ya soksi kwa sharti nne:

1 – Soksi hiyo iwe safi. Lau soksi hiyo itakuwa inatokamana na ngozi [ya mnyama] najisi, si sahihi kupangusa juu yake. Najisi ni kitu kichafu na hakisafiki vovyote utavyoosha. Na zikishakuwa ni najisi ni jambo lenye kujulikana ya kwamba mtu hawezi akaswali nazo. Hivyo asipanguse juu yake.

2 – Azivae wakati yuko na wudhuu’ wa maji. Akizivaa wakati ambapo alifanya Tayammum, hafai kupangusa juu yake. Kwa mfano mtu ni msafiri na amevaa soksi wakati ambapo alikuwa na twahara ya Tayammum kisha akafika katika mji wake, haifai kwake kupangusa juu yake kwa kuwa alizivaa akiwa na twahara ya Tayammum. Twahara ya Tayammum ina mafungamano na uso na viganjavya mikono. Haina mafungamano na miguu. Kujengea juu ya hili sharti inakuwa ni yenye kuchukuliwa kutoka katika maneno yake Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kumwambia al-Mughiyrah bin Shu´bah:

“Nilizivaa zikiwa na twahara.”[1]

3 – Iwe wakati wa hadathi ndogo au kwa msemo mwingine wakati ambapo alitawadha. Haifai kupangusa juu ya soksi wakati mtu yuko na josho la janaba. Ni lazima kwa mtu kuzivua na aoshe miguu. Kwa mfano mtu akipatwa na janaba hawezi kupangusa juu ya soksi.

4 – Iwe kwa muda maalum uliyowekwa katika Shari´ah: mchana mmoja na usiku wake kwa mkazi na nyusiku tatu kwa msafiri. Wakati wa kupangusa unaanza pale mara ya kwanza unapopangusa baada ya kuchenguka wudhuu’. Muda hauanzi kuhesabiwa midhali hujaanza hujapangusakwa mara ya kwanza.

Kwa mfano mtu amefuta juu ya soksi ilihali ni mkazi na akasafiri kabla ya muda kumalizika, atimize kupangusa kama msafiri kwa siku tatu. Kwa mfano akavaa leo wakati wa Fajr na akapangusa ili aswali Dhuhr, kisha akasafiri baada ya Dhuhr, atimize siku tatu. Ikiwa kinyume; ameanza kupangusa katika hali ya usafiri kisha akawa mkazi [kwa kurudi katika mji wake], atimize kupangusa kama mkazi. Kinachozingatiwa ni kwa kule kumalizia na si kuanzia. Usafiri na ukazi kinachozingatiwa ni kule kumalizia na si kuanzia. Hili ndio alilolipa nguvu Imaam Ahmad (Rahimahu Allaah). Mwanzoni alikuwa akisema mtu akipangusa hali ya kuwa ni mkazi kisha akasafiri, akamilishe kupangusa ilihali ni mkazi. Lakini baadayealijirejea kwa upokezi na kauli hii na akasema badala yake atimize kupangusa kama msafiri. Usishangazwe kuona mwanachuoni anajirejea katika msimamo wake. Haki ndio yenye haki kufuatwa. Pale ambapo haki itambainikia mtu ni wajibu kuifuata. Imaam Ahmad (Rahimahu Allaah) wakati mwingine kunapokelewa kwake zaidi ya kauli nne, tano mpaka saba juu ya sualamoja ilihali ni mtu mmoja. Wakati fulani anaweka wazi mwenyewe kuwa amejirudi na wakati mwingine haweki wazi. Akiweka wazi kuwa amejirudi katika ile kauli yake ya kwanza, haijuzu kumnasibishia ile kauli ya kwanza aliyojirejea kwayo. Vilevile na wala haijuzu kumnasibishia nayo isipokuwa ikiwa kama itakuwa kwa njia ya kuifungamanisha kwa kusema “ilikuwa ni kauli yake ya kwanza kisha baadaye akajirejea”. Ama ikiwa hakuweka wazi kujirejea, ni wajibu kumnasibishia kauli zake zote kwa kusema “ana kauli mbili, tatu au nne”.

[1] Muslim (274).

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Riyaadh-is-Swaalihiyn (01/370-372)
  • Imechapishwa: 17/05/2023