Maana ya kufanya Ilhaad katika majina na sifa za Allaah

Swali: Muuliza huyu kutoka Ufaransa anaomba umuwekee wazi ni nini shirki katika majina na sifa za Allaah? Je, mahala hapa kuna shirki na inakuwa vipi?

Jibu: Ni kufanya Ilhaad katika majina na sifa. Allaah (Jalla wa ´Alaa) amesema:

وَذَرُوا الَّذِينَ يُلْحِدُونَ فِي أَسْمَائِهِ ۚ سَيُجْزَوْنَ مَا كَانُوا يَعْمَلُونَ

“Na waacheni wale wanaopotoa katika majina Yake, watalipwa yale waliyokuwa wakiyatenda.” (07:180)

Miongoni mwa kufanya Ilhaad katika majina ya Allaah ni kumkanushia nayo Allaah (Jalla wa ´Alaa) kama wanavyofanya Mu´attwilah. Vilevile kuyafanyia Ta´wiyl kinyume na maana yake kama wanavyofanya Mu´awwilah. Huku ni katika kufanya Ilhaad. Vilevile kuwaita viumbe kwayo kama walivyoita sanamu al-Laat kutokamana na Allaah, ´Uzzaa kutokamana na ´Aziyz na Manaatah kutokamana na Mannaan. Huku pia ni katika kuyafanyia Ilhaad. Kuna aina mbali mbali za Ilhaad. Inahusiana na kuyakanusha na kuyapinga. Vilevile inahusiana na kuthibitisha matamshi yake na wakati huo huo mtu anapotosha maana yake kwa yale yanayoashiriwa, kuita masanamu kwayo kama al-Laat, ´Uzzaa na Manaatah au kuingiza kitu pamoja na majina na sifa hiyo kisichokuwemo humo. Bi maana ya kwamba mtu akathibitisha majina na sifa ambazo hazikuthibiti katika Qur-aan na Sunnah. Huku ndio kufanya Ilhaad.

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Qaa´idah Jaliylah fiyt-Tawassul wal-Wasiylah (23) http://www.alfawzan.af.org.sa/node/2135
  • Imechapishwa: 11/07/2020