Lau wanazuoni wangelikuwa wanajua kuwa tunafanya tarjama fataawaa zao…

Swali: Baadhi wanasema kuwa iwapo wanazuoni wetu kubwa, kama vile Ibn Baaz, Ibn ´Uthaymiyn, al-Albaaniy na al-Fawzaan, wangelijua kuwa fataawaa zao za ki-Fiqh na za kimfumo zinafanyiwa tarjama kwenda katika lugha nyingine, basi wasingeruhusu jambo hilo kwa sababu fataawaa hizo haziendani na waislamu wanaoishi Magharibi. Je, hilo ni kweli?

Jibu: Hilo si sahihi. Hilo si sahihi. Kwa nini zisiendani na watu wa Magharibi? Ina maana kwamba wanaoishi Magharibi wanazo hukumu mpya zinazoenda kinyume na hukumu walizojibu wanazuoni wetu kwa mujibu wa Qur-aan na Sunnah? Maneno haya si kweli. Madai hayo hayana msingi wowote. Mashaykh walikuwa wakijitahidi hata katika matukio yanayozuka na mapya. Wakati mwingine wanafanya vikao baada ya vingine ili kuweze kufikia kwenye hukumu. Wakati mwingine baadhi yao hunyamaza na kujiweka pembeni. Hebu wacha niwape mfano. Shaykh wetu Muhammad al-Amiyn haoni kufaa kufanya bidii (السعي) kwenye ghorofa za juu katika msikiti Mtakatifu. Walikaa vikao vingi mpaka wanazuoni wengi wakafikia kuona kuwa inafaa. Shaykh wetu Muhammad al-Amiyn as-Shanqitwiy (Rahimahu Allaah) akajiweka pembeni na hakuona kuwa inafaa. Mnajua kuwa wanafanya juhudi kubwa katika kutoa fataawaa, khaswa zinazohusiana na matukio mapya. Hushiriki katika makumi ya vikao kabla ya kutoa fatwa kuhusu upandikizaji wa mimba. Ni vipi basi mtu anaweza kusema kuwa wangelibadilisha fataawaa zao hii leo, zinazoendana yale wanayohitaji waislamu wa Magharibi? Hukumu ni moja.

  • Mhusika: Shaykh Swaalih bin Sa´d as-Suhaymiy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: https://darulhadith.com/om-de-larde-visste-att-vi-oversatte-deras-utslag/
  • Imechapishwa: 04/09/2023