Tofauti ya wanazuoni na wale wanaojivisha majoho na vilemba vya ukoka

Swali: Ni vipi tutatofautisha kati ya wanazuoni wakubwa na wale wanaojifanya ni wanazuoni wanaowapotosha watu kwa fataawaa zao?

Jibu: Kwa mambo yafuatayo:

1 – Kupatiliza na kushikamana kwao na Tawhiyd.

2 – Kulingania kwao katika Qur-aan na Sunnah.

3 – Wanayafanyia kazi.

4 – Wako imara wakati wa fitina. Hawabadiliki kwa kubadilika kwa hali, wakati na zama. Utawaona wanakuwa na msimamo uleule katika masuala mbalimbali ambayo wanayapima kwa Qur-aan, Sunnah, na mfumo wa Salaf ambapo wanafikia natija kutokana na hayo.

5 – Ni wa wazi na hawafichi. Hawawakusanyi watu nyikani au maeneo yaliyojificha. Kwa sababu dini ni kitu kiko wazi, hakuna kitu chenye kujificha. ´Umar bin  ´Abdil-´Aziyz amesema:

“Ukiwaona watu wanajitenga na umma wakizungumza mambo yao ya kidini, basi utambue kwamba wao wanaunda upotovu.”[1]

6 – Hawajali jambo la kuzitangaza nafsi zao:

“Anapokuwa katika kulinda basi hulinda na anapokuwa kwenye timu ya nyuma basi yuko kwenye timu ya nyuma. Akiomba ruhusa basi hapewi ruhusa na akiombea hakubaliwi uombezi wake.”

7 – Wanawapendea ndugu zao yale wanayojipendea nafsi zao wenyewe. Lengo lao ni moja; kuwaongoza viumbe katika kheri:

“Naapa kwa Allaah! Allaah kumwongoza mtu mmoja kupitia kwako ni bora kwako kuliko ngamia wekundu.”[2]

Hizi ni baadhi ya alama za wanazuoni wakubwa ambao tunatakiwa kuwaigiliza.

[1] al-Bukhaariy (2887).

[2] al-Bukhaariy (309) na Muslim (405).

  • Mhusika: Shaykh Swaalih bin Sa´d as-Suhaymiy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: https://youtu.be/53LXRTgFvxA
  • Imechapishwa: 04/09/2023