Swali: Ni upi msimamo juu ya tofauti za wanachuoni ikiwa mmoja wapo atatoa Fatwa juu ya masuala fulani na mwanachuoni mwingine naye akatoa Fatwa kwa masuala hayo hayo, lakini hata hivyo majibu yao yakawa yanatofautiana. Tuchukue maoni ya yupi?

Jibu: Allaah Hakutuacha kwenye maoni na tofauti. Ameturudisha kwenye Qur-aan na Sunnah. Allaah (Jalla wa ´Alaa) Amesema:

فَإِن تَنَازَعْتُمْ فِي شَيْءٍ فَرُدُّوهُ إِلَى اللَّـهِ وَالرَّسُولِ إِن كُنتُمْ تُؤْمِنُونَ بِاللَّـهِ وَالْيَوْمِ الْآخِرِ

“Mkizozana katika jambo basi lirudisheni kwa Allaah na Mtume mkiwa mnamwamini Allaah na Siku ya Mwisho.” (04:59)

Ikiwa una elimu ya kujua dalili kinachokupasa ni kuchukua maoni yaliyosimama juu ya dalili katika Qur-aan na Sunnah na kuacha maoni yasiyokuwa na dalili. Ama ikiwa wewe ni mjinga na hujui dalili, kinachokupasa ni kuwauliza wanachuoni. Usichukue maoni yoyote isipokuwa baada ya kuwauliza wanachuoni waaminifu. Lile watalokujibu ndio uchukue. Ama kuchukua maoni yoyote, sawa ikiwa ni kutoka kwa watu wanaostahiki na wasiostahiki, wajinga na wanachuoni wapotevu, hili halijuzu. Haijuzu kamwe. Ikiwa unaweza kuchagua kauli yenye nguvu kwa dalili fanya hivo. Ikiwa huwezi hili, waulize wanachuoni. Allaah (Jalla wa ´Alaa) Amesema:

فَاسْأَلُواْ أَهْلَ الذِّكْرِ إِن كُنتُمْ لاَ تَعْلَمُونَ

“Basi waulizeni wenye ukumbusho kama nyinyi hamjui.” (16:43)

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Buluugh al-Maraam (36) http://www.alfawzan.af.org.sa/sites/default/files/blug–1431-08-15.mp3
  • Imechapishwa: 21/04/2015