Kutokana na kwamba wazazi wengi wanalalamika juu ya kwamba watoto wao wanapuuzia swalah na hawawezi kuwaamsha, ndipo nikapendelea kuandika barua hii ili kuwanasihi watoto wetu. Allaah awafanye waweze kutufurahisha, awarekebishe na awafanye ni miongoni mwa wale wenye kusimamisha swalah.

بسم الله الرحمن الرحيم

السلام عليكم و رحمة الله و بركاته

Hii ni barua ya ukumbusho wa kimapenzi, moja kwa moja kutoka kwa baba aliye na moyo wa huruma.

Mwanangu kipenzi! Tambua ya kwamba swalah ndio jambo muhimu sana katika maisha ya mja. Yule mwenye kuihifadhi basi ameihifadhi dini yake. Na yule mwenye kuipuuza basi atayapuuza mambo mengine vibaya zaidi. Swalah ndio nguzo ya Uislamu. Swalah ikikubaliwa basi matendo mengine yote yanakubaliwa. Swalah ikikataliwa, basi matendo mengine yote yanakataliwa. Swalah ndio faradhi ya kwanza ya Uislamu na ndio jambo la mwisho linalopotezwa katika dini. Swalah ndio jambo la kwanza katika Uislamu na ndio vilevile jambo la mwisho. Dini na matendo ya muislamu hayawi sahihi na njia zake katika mambo ya dini na ya dunia yake hayasimami sawa sawa isipokuwa mpaka asimamishe swalah hii kwa njia iliyowekwa katika Shari´ah.

Mwanangu kipenzi! Tambua ya kwamba wewe utakuja kusimama mara mbili mbele ya Mola wako; mara ya kwanza ni katika dunia hii na mara ya pili ni siku ya Qiyaamah pindi utapokutana na Mola wako (Jalla wa ´Alaa). Upande mmoja matokeo ya kutengemaa kwa hali yako katika maisha haya kwa kufaulu na kufurahi kwako katika maisha ya hapo kesho. Upande wa pili matokeo ya kuharibika kwa hali ya mja katika maisha haya kwa kupoteza na kuhasirika hali yake katika maisha ya hapo kesho.

Hali ya kwanza ni swalah hii ambayo Allaah (Ta´ala) ameiwajibisha juu ya waja Wake na akawafaradhishia nayo mchana na usiku. Yule atakayeichunga swalah hii na akaitilia umuhimu na akaitekeleza kwa wakati wake na akachunga sharti zake, nguzo zake na mambo yake ya wajibu basi atakuwa na hali nyepesi siku ya Qiyaamah; atafaulu na kuokoka. Na yule atakayechukulia wepesi hali hii na akaipuuzisha swalah, asiidhibiti na wala asichunge nguzo zake, sharti zake wala yale mambo yake ya wajibu basi hali yake itakuwa nzito na ya kutatanisha siku ya Qiyaamah.

at-Tirmidhiy, an-Nasaa´iy na wengineo wamepokea kupitia kwa Hurayth bin Qabiyswah (Rahimahu Allaah) ambaye amesema:

“Nilifika al-Madiynah na nikamuomba Allaah (Ta´ala) anipe watu wazuri wa kutangamana nao. Nikakaa na Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu ´anh) na kumwambia: “Ee Abu Hurayrah! Mimi nilimuomba Allaah anipe watu wazuri wa kutangamana nao. Nifunze Hadiyth uliyoisikia kutoka kwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) huenda Allaah akaninufaisha kwayo. Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu ´anh) akasema: “Nilimsikia Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akisema:

“Jambo la kwanza ambalo Allaah atamuhesabu nalo mja katika matendo yake ni swalah; ikisihi, basi amefaulu na kuokoka, na ikiharibika, basi ameangamia na kuhasirika.”

Hadiyth ni Swahiyh.

Zingatia namna ambavyo usalama wa hali ya pili inatokamana na usalama ya hali ya kwanza na jinsi ambavyo hasara ya hali ya pili inatokamana na hasara ya hali ya kwanza. Mche Allaah juu ya swalah. Ichunge hali hii mbele ya Allaah (Jalla wa ´Alaa). Iadhimishe swalah, basi utaadhimika na kupandishwa ngazi mbele ya Allaah.

Mwanangu kipenzi! Allaah akikutunuku kwa kukupa baba ambaye anakujali kwa swalah hii, anakuhimiza na kukupa moyo kwayo, basi nakuonya na tena nakuonya usije kumkasirikia au kukereka naye kwa vile anakufuatilia. Hafanyi hivo kwa jengine isipokuwa tu ni kwa sababu anataka kukuokoa kutokamana na hasira za Allaah na kukufanya uweze kupata radhi za Allaah (Tabaarak wa Ta´ala). Allaah (Jalla wa ´Alaa) hatokuwa radhi na wewe isipokuwa pale utapokuwa ni mwenye kuihifadhi swalah hii na kuitekeleza.

Mwanangu kipenzi! Miongoni mwa kuiadhimisha swalah ni pamoja vilevile na kuamka, kwa furaha, kwa nguvu na kwa kutaka mwenyewe ili kuiswali swalah hiyo pale inaponadiwa. Usiwe uvivu na uzembeaji. Abul-Qaasim al-Aswbahaaniy amepokea katika “at-Targhiyb wat-Tarhiyb” ya kwamba Ibn ´Abbaas (Radhiya Allaahu ´anhumaa) amesema:

“Imechukizwa mtu akaamka kuswali hali ya kuwa na uvivu. Anatakiwa kuswali ilihali ni mwenye tabasamu, hamu na furaha kubwa. Kwani anataka kumnong´oneza Allaah (Jalla wa ´Alaa). Allaah (´Azza wa Jall) yuko mbele yake, anamsamehe na anamuitikia akimuomba.”

Akasoma Aayah hii:

وَإِذَا قَامُوا إِلَى الصَّلَاةِ قَامُوا كُسَالَىٰ

“Wanaposimama kuswali husimama kwa uvivu.”[1]

Uzembe, uchovu na uvivu wakati wa kuswali kunatokamana na udhaifu uliyomo ndani ya moyo wa mja, kuchukulia wepesi na kutokuwa na utambuzi wa thamani na nafasi ya swalah. Kizazi cha kwanza kilitilia umuhimu mkubwa swalah ya mkusanyiko, kiasi cha kwamba Ibn Mas´uud (Radhiya Allaahu ´anh) amesema:

“Tulikuwa (sisi Maswahabah wa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) tukiona hakuna mwenye kuikwepa (swalah ya mkusanyiko) isipokuwa tu mnafiki ambaye unafiki wake unajulikana. Mtu alikuwa anaweza kuburutwa kati ya watu wawili ili aweze kusimamishwa katika safu.”

Endapo mtu hawezi kutembea kwa sababu ya maradhi au utuuzima, basi anashikwa kwenye mabega yake na wanamsaidia kwenda msikitini ili aweze kusimama kwenye safu pamoja na waislamu wenzie na kuswali. Yote haya ni kwa sababu nyoyo zao zilikuwa zinatambua kikweli thamani na nafasi ya swalah. Wakati nafasi ya swalah ilipokuwa kubwa nyoyoni mwao, ndipo miili hii dhaifu sana ikaanza kutikisika kwenda misikitini.

Fajr, inayoanza mwanzoni mwa siku, ina shani maalum. Kuichunga kunapelekea katika mafanikio na furaha ya mtu katika siku yake yote, na kuipoteza kunasababisha kukosa kheri na baraka za siku yote.

Hebu kila mmoja azingatie maana ya yale yaliyothibiti kwa al-Bukhaariy na Muslim kupitia kwa Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu ´anh) ambaye amesimulia kuwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Pindi mmoja wenu anapolala basi shaytwaan anafunga mafundo matatu shingoni mwake. Kila anapofunga fundo moja anasema: “Mbele yako una usiku mrefu; lala.” Anapoamka na kumtaja Allaah, fundo limoja hufunguka. Anapotawadha, basi fundo lingine hufunguka. Anaposwali, fundo lingine hufunguka. Matokeo yake anaamka hali ya kuwa ni mchangamfu na anajihisi vizuri. Vinginevyo anaamka akijihisi vibaya na mvivu.”

Hivi ndivyo inavyokuwa hali ya ambaye haswali Fajr. Anaamka hali ya kuwa na moyo mbaya na siku yake nzima anahisi uvivu, ilihali akiwa ni mwenye kuichunga Fajr na kuiswali kwa wakati wake pamoja na waislamu wenzie basi siku yake inakuwa ni yenye baraka na furaha.

Hebu wacha kila mmoja azingatie tena Hadiyth iliyopokelewa na al-Bukhaariy na Muslim kupitia kwa ´Abdullaah bin Mas´uud (Radhiya Allaahu ´anh) ambaye amesema:

“Kuna mwanamume aliyelala usiku mzima mpaka alipoamka asubuhi alitajwa kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ambapo akasema:

“Huyo ni mwanamme ambaye shaytwaan amekojoa masikioni mwake – au sikioni mwake.”

Wanachuoni wamebainisha kuwa shaytwaan anakojoa sikioni mwake kikweli. Mtu atakuwa namna gani anapoamka akiwa na uchafu wa mikojo yenye kujaa sikioni mwake? Hivyo ndivyo inavyokuwa hali ya ambaye analala fofofo na kupitwa na swalah ya Fajr.

Hebu kila mmoja azingatie Hadiyth iliyopokelewa na al-Bukhaariy kupitia kwa Samurah bin Jundub (Radhiya Allaahu ´anh) katika siyaki ndefu ambapo Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alitaja ndoto aliyoiona na kusema:

“Tulimfikia mwanaume aliyelala ilihali kuna mwengine amesimama juu yake kwenye jiwe. Akamrushia lile jiwe kichwani mwake na kikavunjika. Jiwe lile likaenda mpaka hapa ambapo akalifuata kulichukua. Hakuwahi kumrudilia kabla ya kichwa chake kuwa kawaida tena. Halafu akafanya kama alivyofanya mara ya kwanza.”

Halafu akasema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) mwishoni mwa Hadiyth:

“Kuhusu mwanamume aliyemwendea na kichwa chake kikavunjwa kwa jiwe, ni mwanamume anayeichukua Qur-aan na kuitupilia mbali na badala yake akalala na kuacha swalah za faradhi.”

Kichwa chake ndicho kinaadhibiwa kwa sababu analala ilihali kihakika alitakiwa kuswali. Kwa sababu usingizi unakuwa kichwani.

Mwanangu kipenzi! Wafuate Salaf wema! Wakiy´ bin al-Jarraah amesema:

“Wakati al-A´mash alipofika karibu umri wa miaka sabini alikuwa hajapitwa na ile Takbiyr ya kwanza ya swalah. Kipindi cha miaka yote hii nilimtembelea na sikuwahi kumuona akikidhi Rak´ah hata moja.”

Ghassaan amesema:

“Mtoto wa ndugu yangu Bishr bin Mansuur alinieleza: “Sijawahi kumuona baba yangu mdogo akipitwa na ile Takbiyr ya kwanza ya swalah.”

Sa´iyd bin al-Musayyab amesema:

“Sijawahi kupitwa na ile Takbiyr ya kwnaza ya swalah kwa miaka khamsini. Sijawahi kuona shingo ya mtu katika swalah kwa miaka khamsini.”

Hii ina maana ya kwamba alikuwa akiswali katika ile safu ya kwanza.

Muhammad bin Sam´aan amesema:

“Kwa miaka arubaini sijawahi kupitwa na ile Takbiyr ya kwanza ya swalah pamoja na imamu, isipokuwa tu wakati alipofariki mama yangu. Hapo ndipo nilipopitwa na mkusanyiko.”

Abu Daawuud amesema:

“Ibraahiym as-Swaa´igh alikuwa ni mwanaume mmoja mwema ambaye aliuawa na Abu Muslim huko ´Arandas. Alikuwa anaposhika nyundo na kusikia adhaana, anaiweka pembeni.”

Ibraahiym at-Taymiy amesema:

“Utakapomuona mtu anatilia wepesi kuja katika ile Takbiyr ya kwanza ya swalah, basi tambua kuwa muoshee mikono.”

Mwanangu kipenzi! Swalah ndio nuru ya waumini na mwanga mioyoni mwao. Swalah ndio mafungamano kati ya mja na Mola wake. Endapo swalah ya mja itakuwa kamilifu kwa njia ya kwamba iko na yale mambo ya lazima inayotakiwa kuwa nayo na yale mambo yaliyopendekezwa kukiwemo kuuhudhurisha moyo ambako ndio nundu ya ile swalah yenyewe, basi mja atahisi kwa hakika yuko na amesimama mbele ya Mola wake kwa namna ya mja kuwa mnyenyekevu na mwenye adabu hali ya kuwa ni mwenye kuhudhurisha kila kile anachokisema na anachokifanya. Mwenye kuzama kwa kumnong´oneza Mola wake na maombi kwa Mola wake. Kwa hivyo sio jambo la kushangaza kuona swalah ni moja ya sababu kubwa ya fadhila na kheri zote na vilevile tisho kubwa juu ya machafu na madhambi yote.

Miongoni mwa athari kubwa na matunda ya swalah matukufu ni kuwa hakuna kinachopelekea katika msamaha na kuyafuta madhambi kama inavofanya. al-Bukhaariy na Muslim wamepokea kupitia kwa Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu ´anh) ya kwamba amemsikia Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akisema:

“Hivi mnaonaje lau mtu atakuwa na uchafu na akawa na mto nje ya mlango wake ambapo anaoga mara tano kwa siku atabaki na uchafu wowote?” Wakasema: “Hatobaki na uchafu wowote.” Akasema: “Hivyo ndivyo mfano wa swalah tano; Allaah anayafuta madhambi kwazo.”

Ninamuomba Allaah mkarimu, akuwafikishe kuiadhimisha swalah, kuihifadhi, kuiswali kama inavyotakiwa, aufungue moyo wako, akuwepesishie jambo lako na aiinue daraja yako duniani na Aakhirah. Swalah na salaam zimwendee Mtume wetu Muhammad, kizazi chake na Maswahabah wake.

Baba yako akupendaye

[1] 04:142

  • Mhusika: Shaykh ´Abdur-Razzaaq bin ´Abdil-Muhsin al-´Abbaad
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: http://al-badr.net/muqolat/3343
  • Imechapishwa: 11/02/2017