Imaam an-Nawawiy (Rahimahu Allaah) amesema:

15- Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu ´anh) ameeleza kuwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Anayemwamini Allaah na siku ya Mwisho azungumze [mambo ya] kheri au anyamaze; na yule anayemwamini Allaah na siku ya Mwisho amkirimu jirani yake; na yule anayemwamini Allaah na siku ya Mwisho amkirimu mgeni wake.”

Hii ni dalili inayoonyesha kuwa kunyamaza kunafuatia daraja ya kuzungumza yaliyo ya kheri. Hilo ni kwa sababu mbili:

1- Maamrisho yameanza kwa kuzungumza mambo ya kheri. Amesema (´alayhis-Salaam):

“Azungumze mambo ya kheri.”

Hili ndio chaguo la kwanza na ambalo mtu anatakiwa kujitahidi kwanza.

2- Daraja ya pili ni kuwa ikiwa hakupata mambo ya kheri ya kuzungumza, basi na anyamaze. Hili ni kwa sababu mtu atafanyiwa hesabu kwa yale anayozungumza. Allaah (Jalla wa ´Alaa) Amesema:

لَّا خَيْرَ فِي كَثِيرٍ مِّن نَّجْوَاهُمْ إِلَّا مَنْ أَمَرَ بِصَدَقَةٍ أَوْ مَعْرُوفٍ أَوْ إِصْلَاحٍ بَيْنَ النَّاسِ

“Hakuna kheri katika minong’ono yao mingi isipokuwa anayeamrisha swadaqah, au mema au kupatanisha baina ya watu.” (04:114)

Kuzungumza mambo ya kheri yanahusiana na mambo matatu katika Kauli Yake (Subhanaahu wa Ta´ala) kwenye Aayah ya Suurah an-Nisaa´:

لَّا خَيْرَ فِي كَثِيرٍ مِّن نَّجْوَاهُمْ إِلَّا مَنْ أَمَرَ بِصَدَقَةٍ أَوْ مَعْرُوفٍ أَوْ إِصْلَاحٍ بَيْنَ النَّاسِ

“Hakuna kheri katika minong’ono yao mingi isipokuwa anayeamrisha swadaqah, au mema au kupatanisha baina ya watu.”

  • Mhusika: Shaykh Swaalih bin ´Abdil-´Aziyz Aalush-Shaykh
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh al-Arba´iyn an-Nawawiyyah, uk. 238
  • Imechapishwa: 14/05/2020