Imaam an-Nawawiy (Rahimahu Allaah) amesema:

وعن أبي حمزة أنس بن مالك الأنصاري – خادم رسول الله صلي الله عليه وسلم – رضي الله عنه قال: قال رسول الله صلي الله عليه وسلم: ((لله أفرح بتوبة عبده من أحدكم: سقط على بعيره، وقد أضله في أرض فلاة)) (متفق عليه)

15 – Hamzah Anas bin Maalik al-Answaariy (Radhiya Allaahu ´anh) – mtumishi wa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) – amesimulia kuwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Allaah ni mwenye furaha mno kwa tawbah ya mja Wake kuliko mmoja wenu aliyeanguka kutoka juu ya ngamia wake na akampotea pindi alipokuwa katika ardhi ya jangwa.”[1]

Katika upokezi wa Muslim imekuja:

“Allaah ni mwenye furaha mno kwa tawbah ya mja Wake wakati anapotubia Kwake kuliko mmoja wenu aliyeanguka juu ya ngamia katika ardhi ya jangwa. Ngamia yule akamkimbia naye amebeba chakula na kinywaji chake. Hivyo akakata tamaa [ya kumpata]. Akaenda chini ya mti kwenye kivuli na huku ameshakata tamaa ya kumpata ngamia yake. Alipokuwa katika hali hiyo ghafla akamuona imesimama mbele yake. Akamshika [mbio] kamba yake. Kisha akasema kutokana na furaha kubwa: “Ee Allaah! Hakika wewe ndiye mja wangu na mimi ndiye mola Wako!” Amekosea kutokana na furaha kubwa.””

Katika Hadiyth hii kuna dalili mtu akikosea katika maneno, hata kama itakuwa ni maneno ya kufuru, ulimi umemteleza, haadhibiwi kwa hilo. Mtu huyu ametamka maneno ya kufuru. Mtu kumwambia Mola Wake “Wewe ndiye mja wangu na mimi ndiye mola Wako!” ni kufuru isiyokuwa na shaka. Lakini kwa vile yalimtoka kwa kuteleza kutokana na furaha kubwa aliyokuwa nayo, alikosea pasi na kujua yanayomtoka mdomoni, hivyo akawa sio mwenye kuadhibiwa. Hivyo mtu likimponyoka neno la kufuru haadhibiwi kwalo. Hili linahusu pia maneno mengine.Kwa mfano mtu atamtukana mwingine kwa njia ya kukosea pasina kukusudia, mtu akamtaliki mke wake kwa njia ya kukosea pasina kukusudia, au akamwachia huru mtumwa wake kwa njia ya kukosea bila ya kukusudia, yote haya hayepelekei katika lolote. Mtu hakukusudia kufanya hivo. Hii ni kama kiapo cha upuuzi. Allaah (Ta´ala) amesema:

لَّا يُؤَاخِذُكُمُ اللَّـهُ بِاللَّغْوِ فِي أَيْمَانِكُمْ وَلَـٰكِن يُؤَاخِذُكُم بِمَا كَسَبَتْ قُلُوبُكُمْ

“Allaah hatokuchukulieni [kukuadhibuni] kwa viapo vyenu vya upuuzi lakini atakuchukulieni kwa yaliyochuma nyoyo zenu.” (02:225)

Hili ni tofauti na mwenye kufanya maskhara. Yule mwenye kufanya istihzai anakufuru akitamka maneno ya kufuru hata kama atakuwa ni mwenye kufanya mzaha. Allaah (Ta´ala) amesema:

وَلَئِن سَأَلْتَهُمْ لَيَقُولُنَّ إِنَّمَا كُنَّا نَخُوضُ وَنَلْعَبُ ۚ قُلْ أَبِاللَّـهِ وَآيَاتِهِ وَرَسُولِهِ كُنتُمْ تَسْتَهْزِئُونَ لَا تَعْتَذِرُوا قَدْ كَفَرْتُم بَعْدَ إِيمَانِكُمْ

“Ukiwauliza bila shaka watasema: “Hakika tulikuwa tunaporoja na tunacheza.” Sema:  Je, mlikuwa mnamfanyia istihizai Allaah na Aayah Zake na Mtume Wake? Msitoe udhuru. Hakika mmekwishakufuru baada ya kuamini kwenu.” (09:65-66)

Mwenye kufanya istihzai amekusudia kutamka na maana yake, lakini hata hivyo ni kwa njia ya maskhara na mzaha na ndio maana anakuwa kafiri. Hili ni tofauti na mtu ambaye hakukusudia ambapo maneno yake hayazingatiwi kuwa ni kitu. Hii ni katika rehema za Allaah (´Azza wa Jall).

[1] al-Bukhaariy na Muslim.

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Riyaadh-is-Swaalihiyn (01/103)
  • Imechapishwa: 06/02/2023