Kukusanya Rak´ah nne kwa Tasliym moja katika Tarawiyh

Swali: Baadhi ya maimamu katika swalah ya Tarawiyh wanakusanya Rak´ah nne au zaidi kwa Tasliym moja bila kukaa chini baada ya Rak´ah mbili na wanadai kwamba kufanya hivo ni katika Sunnah. Je, kitendo hichi kina msingi katika Shari´ah takasifu?

Jibu: Kitendo hichi hakikuwekwa katika Shari´ah. Bali kinachukiza au haramu kwa mtazamo wa wanazuoni wengi. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Swalah ya usiku ni [Rak´ah] mbilimbili.”

Ameipokea al-Bukhaariy na Muslim kupitia kwa Ibn ´Umar (Radhiya Allaahu ´anhumaa).

Pia kutokana na yale yaliyothibiti kupitia kwa ´Aaishah (Radhiya Allaahu ´anhaa) ambaye amesimulia:

“Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alikuwa akiswali usiku Rak´ah kumi na moja na akitoa salamu kila baada ya [Rak´ah] mbili na akiswali Witr kwa [Rak´ah] moja.”

Ameipokea al-Bukhaariy na Muslim.

Ziko Hadiyth nyingi zenye maana kama hii. Kuhusu Hadiyth inayotambulika:

“Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alikuwa akiswali usiku [Rak´ah] nne. Usiulize juu uzuri na urefu wake, kisha akiswali [Rak´ah] nne. Usiulize juu uzuri na urefu wake.”

makusudio ni kwamba alikuwa akitoa Tasliym kila baada ya Rak´ah mbili. Makusudio si kwamba alikuwa akiswali zote tatu kwa pamoja kwa Tasliym moja kutokana na Hadiyth yake iliyotangulia. Vilevile imethibiti kutoka kwake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kwamba amesema:

“Swalah ya usiku ni [Rak´ah] mbilimbili.”

Kama tulivyotangulia kusema. Hadiyth zinasadikishana na baadhi zinafasiri zingine. Kwa hivyo ni wajibu kwa muislamu kuzitendea kazi zote na kufasiri zisizokuwa wazi kwa zilizo wazi.

  • Mhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Majmuu´-ul-Fataawa (30/38)
  • Imechapishwa: 10/04/2023