Kujikweza – sifa mbaya ya vijana wengi wa leo

Naona kwamba ushauri unaotolewa na ndugu yetu tunapaswa kuufanyia kazi. Tunaishi katika zama ambazo sifa moja mbaya inayoweza kuangamiza imethibitika, nayo ni kwamba kila mmoja kuvutiwa na maoni yake mwenyewe. Leo hii mara nyingi mtu hujifunza baadhi ya masuala au kuelewa kidogo kutoka ndani ya Qur-aan na Hadiyth chache za Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na kisha anajidhania kuwa amepata elimu fulani. Sisemi kwamba mtu huyo anajidhania kuwa ni kiongozi wa elimu, bali hawezi hata kusoma Hadiyth moja bila kufanya makosa ya kisarufi, achilia mbali kuielewa kwa ufahamu wa kiarabu ulio sahihi. Kisha mtu huyo anajitwika bendera ya mijadala na mabishano juu ya suala ambalo hajawahi kulijua au kufuatilia kwa kina. Hali ya ulimwengu wa Kiislamu leo ni ya kusikitisha… Mimi ni mwenye kukumbusha sasa, si mwenye kujadiliana. Mjadala umekwisha. Nakukumbusha Hadiyth ya Hudhayfah kwa makini, na usiseme kuwa umeisoma na kuielewa kwa msingi wa mazungumzo yetu. Nakukumbusha tu, kukuzindua kama kijana mwenye wivu juu ya dini yake ya kwamba Uislamu umewagawanya watu makundi mawili: wanazuoni na wasiokuwa wasomi. Amesema (Ta´ala) katika Aayah inayotambulika:

فَاسْأَلُواْ أَهْلَ الذِّكْرِ إِن كُنتُمْ لاَ تَعْلَمُونَ

“Basi waulizeni wenye ukumbusho kama nyinyi hamjui.”[1]

Kila mmoja wetu anapaswa kutambua nafasi yake ambayo Allaah amemuweka; yeye ni mwanachuoni, mwanafunzi, msikilizaji au aliyeangamia? Mtu akijitathmini na kugundua kuwa yeye si mwanachuoni wa dini, labda hata si mwanafunzi wa dini, basi haifai kwake kujiingiza kwenye masuala mazito ya dini na akaanza kulingania katika mambo ambayo watu wakimfuata basi atawapoteza na kuwaangamiza.

[1] 16:43

  • Mhusika: Immaam Muhammad Naaswir-ud-Diyn al-Albaaniy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Fataawaa ´abr-al-Haatif was-Sayyaarah (2)
  • Imechapishwa: 09/12/2024