Kufungua swawm ya kulipa baada ya kiu na njaa kali

Swali: Siku moja nilinuia kufunga deni langu la Ramadhaan lakini hata hivyo sikukamilisha kwa sababu nilihisi kiu. Nikafungua kwa kujengea kwamba nitafunga siku ya kufuatia. Lakini marafiki zangu walinilaumu sana na wakanieleza kuwa nilichokifanya ni haramu. Uhakika wa mambo ni kwamba sikuwa najua jambo hilo khaswa ikiwa si ndani ya Ramadhaan na nikadhani kuwa jambo ni lenye wasaa. Nifanye nini?

Jibu: Ndio. Yale uliyoambiwa na dada zako ndio ya sawa. Haijuzu kwako kula kwa sababu tu ya kuhisi njaa. Unalazimika kuwa na subira mpaka lizame jua. Kwa sababu kulipa siku zako za Ramadhaan ni faradhi na hivyo haijuzu kuchukulia wepesi. Mtu akihisi njaa au kiu ilihali amefunga swawm ya faradhi, afanye subira na astahamili mpaka aikamilishe. Isipokuwa ikiwa atachelea kufa au maradhi makali ambapo anaona kuwa hali inapelekea huko. Katika hali hiyo atakuwa na udhuru wa kufungua. Ale tu kile kiasi kitamwaondoshea khatari hiyo kisha ajizuilie mpaka wakati wa kuzama kwa jua. Ama kuhisi njaa au kiu kidogo ambacho hakipelekei katika khatari yoyote, haimjuzishii mtu kufungua funga ya faradhi; si ndani ya Ramadhaan, wakati wa kulipa swawm ya Ramadhaan, swawm ya nadhiri wala swawm ya kafara. Bali analazimika kujizuilia na kufanya subira mpaka jua lizame. Aidha unapaswa kutubu kwa Allaah, kuomba msamaha na kulipa siku hiyo.

  • Mhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: https://binbaz.org.sa/fatwas/11228/حكم-الافطار-في-صوم-القضاء
  • Imechapishwa: 25/03/2023