02. Dalili ya kwanza juu ya kufaradhishwa kufunga Ramadhaan

Kufunga Ramadhaan ni wajibu na faradhi miongoni mwa faradhi zake za Uislamu kuu. Aidha ni moja miongoni mwa nguzo zake za Uislamu tano. Msingi wa ulazima wake ni Qur-aan, Sunnah na maafikiano. Dalili kuhusu ulazima na faradhi yake ziko dhahiri na wazi na zenye kutambulika kwa wasiokuwa wasomi, sembuse wasomi.

Swawm ilifaradhishwa katika mwaka wa pili baada ya kuhajiri ambapo Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akafunga Ramadhaan tisa kwa maafikiano. Waislamu wameafikiana juu ya ulazima wa kufunga Ramadhaan. Allaah ameufaradhishia ummah wa Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kufunga mwezi mmoja kila mwaka, nao ni mwezi wa Ramadhaan. Miongoni mwa dalili za ulazima wake ni yale yafuatayo:

1 – Allaah (Ta´ala) amesema:

يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا كُتِبَ عَلَيْكُمُ الصِّيَامُ كَمَا كُتِبَ عَلَى الَّذِينَ مِن قَبْلِكُمْ لَعَلَّكُمْ تَتَّقُونَ أَيَّامًا مَّعْدُودَاتٍ ۚ فَمَن كَانَ مِنكُم مَّرِيضًا أَوْ عَلَىٰ سَفَرٍ فَعِدَّةٌ مِّنْ أَيَّامٍ أُخَرَ ۚ وَعَلَى الَّذِينَ يُطِيقُونَهُ فِدْيَةٌ طَعَامُ مِسْكِينٍ ۖ فَمَن تَطَوَّعَ خَيْرًا فَهُوَ خَيْرٌ لَّهُ ۚ وَأَن تَصُومُوا خَيْرٌ لَّكُمْ ۖ إِن كُنتُمْ تَعْلَمُونَ شَهْرُ رَمَضَانَ الَّذِي أُنزِلَ فِيهِ الْقُرْآنُ هُدًى لِّلنَّاسِ وَبَيِّنَاتٍ مِّنَ الْهُدَىٰ وَالْفُرْقَانِ ۚ فَمَن شَهِدَ مِنكُمُ الشَّهْرَ فَلْيَصُمْهُ ۖ وَمَن كَانَ مَرِيضًا أَوْ عَلَىٰ سَفَرٍ فَعِدَّةٌ مِّنْ أَيَّامٍ أُخَرَ ۗ يُرِيدُ اللَّـهُ بِكُمُ الْيُسْرَ وَلَا يُرِيدُ بِكُمُ الْعُسْرَ وَلِتُكْمِلُوا الْعِدَّةَ وَلِتُكَبِّرُوا اللَّـهَ عَلَىٰ مَا هَدَاكُمْ وَلَعَلَّكُمْ تَشْكُرُونَ

“Enyi mlioamini! Mmeandikiwa [fardhi ya] swawm kama ilivyoandikwa kwa walio kabla yenu mpate kuwa na taqwa. [Kufunga swawm kwenyewe ni] siku za idadi maalum. Basi atakayekuwa mgonjwa miongoni mwenu, au yuko safarini [akafunga baadhi ya siku], basi [akamilishe] idadi [ya siku anazotakiwa kufunga] katika siku nyinginezo. Na ni juu ya wale wanaoiweza [kufunga swawm] lakini kwa tabu watoe fidia kulisha masikini. Na atakayejitolea kwa jema lolote lile basi ni bora kwake, na mkifunga swawm ni bora kwenu – mkiwa mnajua [ni ubora kiasi gani kwa nyinyi kufanya hivo]! Mwezi wa Ramadhaan ambao [kumeanzwa] kuteremshwa humo Qur-aan ili iwe mwongozo kwa watu na hoja bayana za mwongozo na pambanuo [la haki na ubatilifu]. Basi atakayeshuhudia miongoni mwenu mwezi [mpya] na afunge  swawm. Na atakayekuwa mgonjwa au safarini basi [atimize] idadi katika siku nyinginezo. Allaah Anakutakieni mepesi na wala Hakutakieni magumu. [Fungeni siku mlizowekewa] ili mkamilishe idadi na ili mumkabiri Allaah kwa kuwa Amekuongozeni na mpate kushukuru.”[1]

Imethibiti katika al-Bukhaariy na Muslim kupitia kwa Ibn ´Umar (Radhiya Allaahu ´anhumaa) aliyesimulia kuwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Uislamu umejengeka juu ya mambo matano: Kushuhudia ya kwamba hapana mungu wa kweli isipokuwa Allaah na kwamba Muhammad ni Mtume wa Allaah, kusimamisha swalah, kutoa zakaah, kuhiji Nyumba na kufunga Ramadhaan.”[2]

Katika Hadiyth hii tukufu ni kwamba Uislamu umejengeka juu ya misingi tano na kwamba kufunga Ramadhaan ni msingi na nguzo ya nne ambao Uislamu umesimama juu yake.

[1] 02:183-185

[2] al-Bukhaariy (08) na tamko ni lake, na Muslim (16).

  • Mhusika: ´Allaamah ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah ar-Raajihiy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: al-Ilmaam bishay´ min Ahkaam-is-Swiyaam, uk. 09-10
  • Imechapishwa: 24/03/2023