Kuchelewesha kuoga na swalah kwa kukosa nguo na baridi kali

Swali: Niliota na ukafika wakati wa swalah ya Fajr. Sikuweza kuoga kutokana na kukosa nguo na baridi kali. Nikaacha mpaka ilipofika swalah ya Dhuhr ndipo nilipata nguo na kuweza kujitwahirisha. Ni ipi hukumu?

Jibu: Anachotakiwa kufanya asiposahilikiwa kupata maji yaliyopashwa moto wala mavazi afanye Tayammum kwa udongo. Apige udongo kwa mikono yake kwa nia ya janaba na nia ya hadathi ndogo ambayo ni wudhuu´. Aidha afute uso wake na viganja vya mikono hali ya kunuia janaba na wudhuu´ vyote viwili. Aswali kutegemea hali yake. Asicheleweshe swalah kwa hali yoyote. Akiichelewesha anapata dhambi. Katika hali hiyo atalazimika kuoga na kulipa swalah anayodaiwa. Lakini analazimika kuswali ndani ya wakati wake ijapo ni kwa Tayammum. Akiweza kuyapasha moto maji na kupata mavazi yatayomsaidia kupata joto, basi atalazimika kufanya hivo. Vinginevyo ataswali kwa kufanya Tayammum na wala asicheleweshe swalah nje ya wakati wake.

  • Mhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: https://binbaz.org.sa/fatwas/3796/حكم-من-اخر-الغسل-والصلاة-لشدة-البرد
  • Imechapishwa: 02/06/2022