Kuamka kwako kula daku ndio nia yenyewe

Swali: Je, ni wajibu kuweka nia ya kufunga Ramadhaan kila siku au inatosha kuweka nia moja ya kufunga mwezi mzima?

Jibu: Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Hakika si vyengine kila kitendo kinategemea na nia na kila mmoja atalipwa kutokana na alivyonuia.”

Hapa kuna dalili ya kwamba ni lazima kuweka nia kwa ajili ya matendo. Kinachodhihiri ni kwamba mtu anuie kila siku. Haina maana kwamba aseme:

“Nanuia kufunga siku kadhaa na kadhaa ya Ramadhaan.”

Nia ni yale makusudio. Kuamka kwako kula daku ndio manuizi. Kujizuilia kwako kula na kunywa kunazingatiwa ni nia.

Kuhusu Hadiyth isemayo:

“Yeyote ambaye hakulaza nia usiku hana swawm.”

ni dhaifu ingawa imesahihishwa na baadhi ya wanazuoni. Maoni sahihi ni kwamba ni dhaifu.

  • Mhusika: ´Allaamah Muqbil bin Haadiy al-Waadi´iy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Fadhwaaih wa Naswaaih, uk. 74
  • Imechapishwa: 14/03/2024