Ambaye amekula hali ya kudhani kuwa jua limekwishazama na baadaye ikabaini kuwa halijazama. Wanazuoni wametofautiana kuhusu ulazima wa yeye kulipa swawm hiyo. Wanazuoni wengi wanaona kuwa anapaswa kuilipa siku hiyo. Wamejengea hoja kwa yale aliyopokea Maalik kutoka kwa ´Umar:

“Alikata swawm kisha jua likachomoza.” Akasema: “Ni kosa dogo na tumejitahidi.”

´Abdur-Razzaaq amezidisha katika upokezi wake kwa njia hii:

“Atalipa siku yake hiyo.”

Ana upokezi mwingine mfano wake kupitia kwa Handhwalah kutoka kwa baba yake. Ameipokea Sa´iyd bin Mansuur. Humo imepokelewa kwamba alisema:

“Yule ambaye amefungua miongoni mwenu basi afunge siku nyingine badala yake.”

Vilevile kwa yale aliyopokea Hishaam bin ´Urwah, kutoka kwa Faatwimah, kutoka kwa Asmaa´ bint Abiy Bakr aliyesimulia:

“Siku moja ya mawingu tulifungua wakati wa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) tulifungua swawm kisha baadaye jua likachomoza.” Hishaam akaulizwa: “Je, waliamrishwa kulipa?” Akajibu: “Ni lazima ilipwe.”

Ameipokea al-Bukhaariy.

Kikosi kingine cha wanazuoni wanasema kuwa halazimiki kulipa. Wamejengea hoja juu ya hilo kwa yale aliyopokea Zayd bin Wahb aliyesimulia:

“Nilikuwa nimeketi kwenye msikiti wa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na tukaletewa chombo ndani yake kuna kinywaji kutoka katika nyumba ya Hafswah. Tukanywa tukiona kuwa usiku umeshaingia. Kisha mawingu yakafunguka na tahamaki jua likachomoza tena. Watu wakawa wanasema kuwa walipe siku nyingine badala yake. ´Umar akasema: “Naapa kwa Allaah kwamba hatutoilipa, hatukutenda dhambi.”

Miongoni mwa ambao wameonelea maoni hayo ni Mujaahid, al-Hasan, Ishaaq na Dhwaahiriyyah. Ni moja katika maoni ya Ahmad na akayachagua Shaykh-ul-Islaam Ibn Taymiyyah. Yamesimuliwa maoni haya kutoka kwa ´Urwah pia. Ibn Khuzaymah amesema kuhusu maneno ya Hishaam aliposema:

“Ni lazima ilipwe.”

“Hakuitajia cheni ya wapokezi na wala haikunibainikia kuwa wanalazimika kulipa.”

Ibn Hajar amesema kuhusu maneno ya Hishaam:

“Sijui kama walilipa au hawakulipa.”

Udhahiri wa upokezi huu unapingana na wa kabla yake unaosema:

“Wakaamrishwa kulipa.”

Kuhusu Hadiyth ya Asmaa´ haikuhifadhiwa kuthibiti kulipa wala kupingwa kwake. Amesema katika “al-Furuu´:

“Imesihi kutoka kwa ´Umar juu ya suala hilo mapokezi mawili; moja yanasema kulipa na kuamrishwa jambo hilo, mengine yanasema kuwa hawalipi kwa sababu hawakutenda dhambi. Akaongezea: “Tulikuwa hatujui.”

Kuchukua tahadhari zaidi watu wanapaswa kulipa.

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Ibraahiym Aalush-Shaykh
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Majmuu´-ul-Fataawaa (04/193-194)
  • Imechapishwa: 14/03/2024