Kualika watu wasome Qur-aan ili mtu anyookewe na mambo yake

Swali: Uganda mtu akitaka kumuomba Mola Wake amkunjulie riziki anawaalika baadhi ya wasomi wanahudhuria kwake na kila mmoja anakuja na msahafu wake na wanaanza kusoma; mmoja anasoma Yaa Siyn kwa kuwa ndio moyo wa Qur-aan, wa pili al-Kahf, wa tatu al-Waaqi´ah, ar-Rahmaan, ad-Dukhaan, al-Ma´aarij, Nuun, al-Mulk, Muhammad, Fath au nyinginezo katika Suurah za Qur-aan. Hawasomi al-Baqarah wala an-Nisaa´. Baada ya hapo wanaomba du´aa. Je, mfumo huu umewekwa katika Uislamu? Ikiwa haukuwekwa tunaomba utueleze mfumo uliyowekwa katika Shari´ah pamoja na dalili.

Jibu: Kusoma Qur-aan pamoja na kuzingatia maana yake ni katika ´ibaadah bora. Kumuomba Allaah du´aa, kurejea Kwake juu ya kufanikiwa katika kheri, kukunjuliwa riziki na kheri nyenginezo ni ´ibaadah iliyowekwa.

Lakini kusoma Qur-aan kwa sura iliyotajwa katika swali ambapo kunagawanywa Suurah maalum kwa watu wengi kutoka katika Qur-aan na kila mmoja anasoma Suurah yake na baada ya hapo kuomba du´aa ya kukunjuliwa riziki na kadhalika ni Bid´ah. Hili halikuthibiti kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) si kwa njia ya maneno wala vitendo. Vilevile halikuthibiti kutoka kwa Swahabah yeyote (Radhiya Allaahu ´anhum) na maimamu wa Salaf (Rahimahumu Allaah). Kheri inapatikana kwa kuwafuata Salaf na shari inapatikana kwa waliokuja nyuma kuzua. Imethibiti kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ya kwamba amesema:

“Mwenye kuzua katika dini yetu hii yasiyokuwemo basi atarudishiwa mwenyewe.”

Kumuomba Allaah du´aa ni jambo limewekwa katika nyakati zote, sehemu zote na katika hali zote sawa za shida na raha. Miongoni mwa sehemu ambazo Shari´ah imekokoteza kuomba du´aa ni katika Sujuud wakati wa swalah, wakati wa daku na mwisho wa swalah kabla ya kutoa Salaam. Imethibiti ya kuwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Mola Wetu hushuka katika mbingu ya dunia kila usiku kunapobaki thuluthi ya mwisho na anasema: “Ni nani mwenye kuniomba du´aa nimuitikie? Ni nani mwenye kuniomba nimpe? Ni nani mwenye kuniomba msamaha nimsamhe.”

Ameipokea al-Bukhaariy na Muslim.

Ibn ´Abbaas (Radhiya Allaahu ´anhumaa) amesimulia ya kuwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Katika Rukuu´ muadhimisheni Mola na katika Sujuud jitahidini kwa du´aa.”

Ameipokea Ahmad, Muslim, an-Nasaa´iy na Abu Daawuud.

Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu ´anh) amesimulia kwamba Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Mahali ambapo mja anakuwa karibu na Mola Wake ni pale anapokuwa amesujudu. Hivyo kithirisheni du´aa.”

Ameipokea Muslim, Abu Daawuud na an-Nasaa´iy.

al-Bukhaariy na Muslim wamepokea kupitia kwa Ibn Mas´uud (Radhiya Allaahu ´anh) ambaye ameeleza kuwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) baada ya kumfunza Tashahhud akamwambia:

“Kisha una khiyari ya kuomba du´aa uitakayo ambayo itaitikiwa.”

  • Mhusika: al-Lajnah ad-Daaimah
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Fataawaa al-Lajnah ad-Daaimah (2/345-346)
  • Imechapishwa: 23/08/2020