Swali: Baadhi ya ndugu wanasema kuwa ni lazima kwa kila muislamu mwenye uwezo kuwalingania makafiri na kwamba inafaa kwa muislamu kuishi kati ya makafiri na kujifananisha nao kwa lengo la ulinganizi na kwamba ulingano huu hauhitaji elimu wala ufahamu. Wamejengea dalili maneno yake Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam): 

”Fikisheni kutoka kwangu ijapokuwa Aayah moja.” 

Ni upi usahihi wa maneno yao? 

Jibu: Haijuzu kuishi kati ya washirikina ikiwa mtu hawezi kudhihirisha dini yake. Katika hali hiyo haijuzu kuishi kati yao. Isipokuwa ikiwa kama anaweza kudhihirisha dini yake, kudhihirisha kuabudiwa kwa Allaah pekee, swalah na matendo mengine ya kheri. Haijuzu kujifananisha na makafiri hata ikiwa ni kwa lengo la kuwalingania. Haijuzu kujifananisha nao. Hata hivyo atawalingania kwa kiasi cha elimu yake kwa kuwaambia watamke shahaadah, wafanyie kazi maana ya shahaadah, awafunze maana ya shahaadah kwa kiasi cha elimu yake na awafunze faradhi za dini. Haijalishi kitu hata kama hana elimu kubwa, atalingania kwa mujibu wa elimu yake: 

”Fikisheni kutoka kwangu ijapokuwa Aayah moja.” 

Awafunze Qur-aan. Makafiri hao wakikubali kusilimu awaambie watamke shahaadah, wamwamini Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam), wamfate na awafunze yale ambayo Allaah amemtunuku kwa kiasi cha wepesi wake. Lakini kama kuna ambaye ana elimu zaidi basi amtake msaada ili mtu huyo afikishe kwa ukamilifu zaidi. Kila ambavyo ufikishaji utakuwa kamili zaidi ndivo utakuwa na manufaa zaidi kwa anayefikishiwa na thawabu kubwa zaidi. Vinginevyo mtu anatakiwa kufikisha kwa kiasi cha uwezo wake. 

  • Mhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Majmuu´-ul-Fataawaa (28/132)
  • Imechapishwa: 08/11/2023