Kila kinachotokea ni kwa makadirio ya Allaah

Kuna faida kubwa sana ya kuamini Qadar. Hilo humfanya mtu akapumzika. Pale anapojua kuwa kila kitu ni lazima kipitike kama alivyoamrisha Allaah, basi atapumzika. Akifikwa na madhara atakuwa na subira na kusema hili ni kutoka kwa Allaah. Akifikwa na ya kumfurahisha atashukuru na kusema haya ni kutoka kwa Allaah. Imethibiti kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ya kwamba amesema:

“Ajabu iliyoje juu ya jambo la muumini!Hakika mambo yake yote ni kheri. Akifikwa na mazuri basi anashukuru na hilo linakuwa ni kheri kwake. Akifikwa na madhara anasubiri na hilo linakuwa ni kheri kwake.”[1]

Kwa sababu muumini anaamini kuwa kila kitu kinapitika kwa makadirio ya Allaah. Basi siku zote anakuwa kwenye furaha na mwenye kufunguka [moyo wake]. Kwa sababu anajua yenye kumfika yanatoka kwa Allaah. Ikiwa ni madhara anasubiri na huku anataraji faraja kutoka kwa Allaah na kumtegemea Allaah (Ta´ala) amtatulie matatizo haya. Na ikiwa ni mazuri basi anashukuru na kumhimidi Allaah na kujua kuwa hayo hayakutokamana kwa uwezo na nguvu zake, bali ni kutokamana na fadhilah na rehema Zake.

[1] Muslim (2999).

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Riyaadh-is-Swaalihiyn (01/477)