Ama Jamaa´at-ut-Tabliygh naona kuwa wako na ujinga mwingi. Na kwamba baadhi ya washupavu huwezi kubadili maoni yao. Mbali na hilo wako pia na kheri nyingi kuhusiana na tabia na kuabudu. Wapotofu na mafasiki wangapi wameongoka kupitia mikono yao? Na haya yako mengi. Hali kadhalika ni makafiri wangapi wamesilimu kupitia mikono yao? Wako na kheri na shari. Lakini wanapelekwa na ujinga.

Na baadhi yao kama nilivyowaambia ni wapinzani, hata ukiwabainishia haki hawakubali kutoka kwako. Nafikiria wale ambao tuko nao hapa Saudi Arabia sijui kama ´Aqiydah yao ina kasoro. Ukiwauliza unamwamini Allaah, Malaika, vitabu Vyake, Mitume Wake na Siku ya mwisho; wanasema “ndio”. Ukiwauliza unaamini kuwa nguzo za Uslamu ni tano, wanasema “ndio”. Lakini kama nilivyowambia wanapelekwa na ujinga, na kwa ujinga wao wameenda kupanga kanuni sita katika manhaj yao. Utaratibu huu ni makosa. Ingelikuwa bora wangepanga katika manhaj yao yale aliyosema Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ndio Dini, wakati Jibriyl alipokuja na kumuuliza Mtume (´alayhis-Salaam) kuhusu Uislamu, imani, ihsaan, Qiyaamah na alama zake. Kisha akasema mwisho wa Hadiyth:

“Huyu ni Jibriyl kaja kwa ajili ya kuwafunza dini yenu.”

Wangeliacha kanuni hizi sita, nazo ni kanuni wamechukua katika Qur-aan na Sunnah lakini ni finyu. Lau wangeziacha na wakajaalia msingi wa manhaj yao ni Hadiyth ya Jibriyl ingelikuwa bora na afadhali kwao. Mimi siwakatazi, lakini naona wanafunzi watoke nao kwa ajili ya kuwasahihisha na kuwafunza. Kwa kuwa wanaathiri watu, taathira ambayo sijui kuna mwengine anayeathiri kama wafanyavyo; kwa kuwaongoza mafasiki, makafiri. Kwa kuwa ni walaini na si wakali katika Da´wah. Lakini akija mtu kuniuliza unaonaje nitoke nao au nitafute elimu, nitamwambia baki na utafute elimu. Usiache kutoka kwako nao ikakuzuia kutafuta elimu.

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih Ibn ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: http://youtu.be/aVkjobJdylA
  • Imechapishwa: 03/09/2020