Josho la janaba kwa mujibu wa Shari’ah

Josho lenye kutosheleza ni mwili wako mzima uweze kupata maji. Ni mamoja ikiwa utaanza kwa kichwa, kifua, mgongo, chini ya mwili au ukajiingiza ndani ya bwawa na ukatoka kwa kunuia kufanya kuoga josho la janaba.

Kutawadha wakati wa kuoga josho la janaba ni sunnah na sio wajibu. Imesuniwa mtu akatawadha kabla ya kuanza kuoga josho la janaba. Akioga hakuna haja ya kutawadha tena kwa mara ya pili kwa sababu haikuthibiti kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kuwa alitawadha baada ya kufanya josho la janaba.

Ikiwa mtu hakupata maji au ni mgonjwa na anaogopa kutumia maji au kuna baridi kali na hana kitu cha kupashia maji, anatakiwa kufanya Tayammum. Allaah (Ta´ala) amesema:

وَإِن كُنتُمْ جُنُبًا فَاطَّهَّرُوا ۚ وَإِن كُنتُم مَّرْضَىٰ أَوْ عَلَىٰ سَفَرٍ أَوْ جَاءَ أَحَدٌ مِّنكُم مِّنَ الْغَائِطِ أَوْ لَامَسْتُمُ النِّسَاءَ فَلَمْ تَجِدُوا مَاءً فَتَيَمَّمُوا صَعِيدًا طَيِّبًا فَامْسَحُوا بِوُجُوهِكُمْ وَأَيْدِيكُم مِّنْهُ

“Mkiwa na janaba, basi jitwaharisheni na mkiwa wagonjwa au mko safarini au mmoja wenu akija kutoka msalani au mmewagusa wanawake kisha hamkupata maji, basi fanyeni Tayammum kwa ardhi kwa juu panguseni kwayo nyuso zenu na mikono yenu.” (05:06)

Allaah akaweka wazi ya kwamba wakati wa safari au ugonjwa mtu afanye Tayammum ikiwa hakupata maji.

Kuhusiana na wakati wa kuogopa baridi, dalili yake ni kisa cha ´Amr bin al-´Aasw (Radhiya Allaahu ´anh) ya kwamba Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alimtuma vitani na akapata janaba. Baada ya hapo akafanya Tayammum na kuwaswalisha wenzake ilihali yeye ndiye imamu. Wakati aliporudi Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akamwambia:

“Ee ´Amr! Hivi kweli umewaswalisha wenzako ilihali una janaba?” Akasema: “Ndio, ee Mtume wa Allaah! Nilikumbuka maneno ya Allaah (Ta´ala):

وَلَا تَقْتُلُوا أَنفُسَكُمْ ۚ إِنَّ اللَّـهَ كَانَ بِكُمْ رَحِيمًا

“Wala msijiue. Kwani hakika Allaah daima kwenu ni Mwenye kurehemu.” (04:29)

Niliogopa baridi nikatawadha udongo msafi kisha ndio nikaswali.”[1]

Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akamkubalia kwa hilo na hakumuamrisha kurudi kuiswali tena. Mwenye kukhofia madhara ni kama aliye na madhara. Kwa sharti awe na khofu kubwa au ya kuonekana. Wasiwasi peke yake hauzingatiwi. 

[1]Abu Daawuud (334).

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Riyaadh-is-Swaalihiyn (01/363-365)
  • Imechapishwa: 15/05/2023