Ni Imaam, Haafidhw na Shaykh-ul-Muhaddithiyn Abu Zakariyyaa Yahyaa bin Ma´iyn bin ´Awn bin Ziyaad bin Bistwaam. Imesemekana vilevile kwamba jina la babu yake ilikuwa Ghayyaath bin Ziyaad bin ´Awn bin Bistwaam al-Ghatwafaaniy, kisha al-Murriy, al-Baghdaadiy – mmoja katika watu maarufu.

Alizaliwa mwaka wa 158.

Baadhi ya ambao amesikia kutoka kwao ni pamoja na Ibn-ul-Mubaarak, Hushaym, Ismaa´iyl bin ´Ayyaash, Sufyaan bin ´Uyaynah, ´Abdur-Razzaaq, Wakiy´, Yahyaa al-Qattwaan, Ibn Mahdiy na wengineo.

Miongoni mwa ambao wamepokea kutoka kwake ni pamoja na Ahmad bin Hanbal, Abu Khaythamah, al-Bukhaariy, Muslim, Abu Daawuud, ´Uthmaan bin Sa´iyd ad-Daarimiy, Abu Zur´ah, Abu Haatim, Abu Ya´laa al-Muusuliy na wengineo.

Ahmad bin Zuhayr amesema:

”Yahyaa amezaliwa 158.”

Alianza kutafuta elimu wakati alipokuwa na miaka 20.

´Abdur-Rahmaan bin Abiy Haatim amesema:

“Nilimsikia baba yangu akiulizwa kuhusu Yahyaa. Akasema: “Ni Imaam.”

an-Nasaa´iy amesema:

“Abu Zakariyyaa ni mmoja katika maimamu wa Hadiyth, mwaminifu na mwenye kuaminiwa.”

al-´Abbaas bin Muhammad amesema:

”Nimemsikia ´Abbaas al-´Anbariy akimuuliza Yahyaa bin Ma´iyn: ”Ee Abu Zakariyyaa! Unatokea katika kabila gani la kiarabu?” Akasema: ”Mimi ni mtumwa niliyeachwa huru wa waarabu.”

Inasemekana kwamba asili ya Ibn Ma´iyn ni kutokamana na Anbaar na alikulia Baghdaad. Ni mmoja katika wale vigogo wakubwa; ´Aliy al-Madiyniy, Ahmad bin Hanbal, Ishaaq bin Raahawayh, Abu Bakr bin Abiy Shaybah na Abu Khaythamah. Walikuwa wakifanya adabu kwake na wakitambua nafasi yake. Alikuwa ni mwenye haiba na utukufu. Alikuwa akipanda nyumbu na akivaa mavazi mazuri – Allaah amrehemu.

Yahyaa amesema:

”Mimi ni huri wa al-Junayd.”

´Aliy al-Madiyniy amesema.

”Elimu huko Baswrah inaishilia kwa Yahyaa bin Abiy Kathiyr na Qataadah, elimu huko Kuufah kwa Abu Ishaaq na al-A´mash na elimu huko Hijaaz kwa Ibn Shihaab na ´Amr bin Diynaar. Baadaye elimu ya watu hawa sita ikaishilia kwa watu kumi na mbili: Ibn Abiy ´Aruubah, Ma´mar, Shu´bah, Hammaad bin Salamah, Sufyaan ath-Thawriy, Sufyaan bin ´Uyaynah, Maalik, al-Awzaa´iy, Ibn Ishaaq, Hushaym, Abu ´Awaanah, Yahyaa bin Sa´iyd, Yahyaa bin Abiy Zaa-idah” … mpaka alipomtaja Ibn-ul-Mubaarak, Ibn Mahdiy na Yahyaa bin Aadam. Baadaye elimu ya watu hawa wote ikaenda kwa Yahyaa bin Ma´iyn.

Ndio, lakini pia Ahmad bin Hanbal, Abu Bakr bin Abiy Shaybah, ´Aliy na wengineo. Kisha baadaye ikaenda kwa al-Bukhaariy, Abu Zur´ah, Abu Haatim, Abu Daawuud na wengineo. Halafu ikaenda kwa Abu ´Abdir-Rahmaan an-Nasaa´iy, Muhammad bin Naswr al-Marwaziy, Ibn Khuzaymah na Ibn Jariyr. Kisha elimu ikaanza kupungua kidogo kidogo.

Kuna bwana mmoja alikuja kwa Ahmad bin Hanbal amesema:

“Ee Abu ´Abdillaah! Itazame Hadiyth hii. Ndani yake kuna kosa.” Akasema: ”Lazimiana na Abu Zakariyyaa. Analijua kosa hilo.”

Ahmad bin Hanbal amesema:

“Kukaa na kumsikiliza Yahyaa bin Ma´iyn ni tiba ya yale yaliyomo ndani ya nyoyo.”

´Aliy bin Sahl amesema:

“Nimemsikia Ahmad bin Hanbal akisema kumwambia ´Abdullaah ar-Ruumiy huko Dihliyz ´Affaan: “Laiti Abu Zakariyyaa angekuja.” Ndipo akasema mtu mmoja: “Utafanya naye kitu gani?” Ahmad akasema: “Nyamaza. Anatambua kosa la Hadiyth.”

Ahmad bin Hanbal akasema:

”Kila Hadiyth asiyoijua Yahyaa bin Ma´iyn basi hiyo si Hadiyth.”

Haaruun bin Ma´ruuf amesema:

”Shaykh alitujia na akaturaukia na tukamuomba kama anaweza kutusomea. Akachukua kitabu na tahamaki kuna mtu anabisha hodi kwenye mlango. Shaykh akasema: ”Ni nani?”Akasema: ”Ahmad bin Hanbal” akampa idhini na Shaykh akabaki katika hali yake. Mwingine akabisha hodi. Shaykh akasema: ”Ni nani?” Akasema: ”Ahmad ad-Dawraqiy” akampa idhini na Shaykh hakutikisika. Kisha akaja Ibn-ur-Ruumiy kisha baadaye akaja Abu Khaythamah. Halafu kukabishwa mlango tena. Akasema: ”Ni nani?” Akasema: ”Yahyaa bin Ma´iyn”. Nikamuona namna ambavo mkono wa Shaykh unatikisika mpaka kitabu kikamdondoka.”

Abu ´Ubayd al-Aajurriy amesema:

“Nilisema kumwambia Abu Daawuud: “Ni nani mjuzi zaidi wa wanamme; Yahyaa au ´Aliy?” Akasema: “Yahyaa.”

´Abdul-Mu´min an-Nasaafiy amesema:

“Nilimuuliza Abu ´Aliy Swaalih bin Muhammad: “Ni nani mjuzi zaidi wa Hadiyth; Yahyaa bin Ma´iyn au Ahmad bin Hanbal?” Akasema: “Ahmad ni mjuzi zaidi wa uelewa na tofauti, kuhusu Yahyaa ni mjuzi zaidi wa wanamme na majina.”

´Aliy al-Madiyniy amesema:

“Sijawahi kuona mtu anayeandika kama Yahyaa bin Ma´iyn.”

Ahmad bin ´Uqbah amesema:

”Nilisema kumwambia Yahyaa bin Ma´iyn: ”Umeandika Hadiyth ngapi?” Akasema: “Nimeandika Hadiyth 600.000 kwa mkono wangu huu.”

Bi maana kwa kuzikariri.

Yahyaa bin Ma´iyn amesema:

”Katu sijawahi kumuona mtu amefanya kosa isipokuwa nilimsitiri na nikapenda kuipamba hali yake. Katu sijawahi kumkabili mtu kwa jambo analolichukia. Hata hivyo humbainishia kosa lake faragha; akikubali ni sawa na vinginevyo humwacha.”

Abu Haatim ar-Raaziy amesema:

“Ukimuona mtu kutoka Baghdaad anampenda Ahmad bin Hanbal, basi tambua kuwa ni mtu anayefuata Sunnah, na ukimuona anamchukia Yahyaa bin Ma´iyn, basi tambua kuwa ni mwongo.”

Muhammad bin Haaruun al-Fallaas amesema:

”Ukimuona mtu anamsema vibaya Yahyaa bin Ma´iyn, basi utambue kuwa ni mwongo ambaye anatunga Hadiyth na si vyenginevyo anamchukia kwa sababu ya kufichua kwake waongo.”

Hubaysh bin Mubashshir amesema:

”Wakati Yahyaa bin Ma´iyn alipokuwa anafanya hijah, alikuwa anaenda Makkah kupitia al-Madiynah na akirudi kupita njia hiyohiyo. Wakati alipofanya hijah yake ya mwisho, alirudi kupitia al-Madiynah na akabaki hapo kwa muda wa siku mbili au tatu. Kisha yeye na marafiki zake wakaondoka na wakapata sehemu wakalala. Usiku akaota mtu anayemwita: ”Ee Abu Zakariyyaa! Hivi unapenda kuwa karibu nami?” Alipoamka akawaambia marafiki zake: ”Endeleeni na safari. Hakika mimi narejea al-Madiynah.” Hatimaye wakaendelea na yeye akarudi nyuma. Akabaki al-Madiynah kwa muda wa siku tatu kisha akafariki. Akabebwa juu ya vijiti ambavyo Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alioshwa kwavyo na watu wakamswalia na kusema: ”Huyu ni mtu ambaye alikuwa akizuia uongo dhidi ya Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam).”

Yahyaa bin Ma´iyn amesema:

”Siku moja tulikuwa katika kijiji miongoni mwa vijiji vya Misri na hatukuwa na chochote wala hakukuwa na chochote cha kununua. Tulipoamka asubuhi, tukaona sahani lililojaa samaki wa kukaanga na halikuwa la yeyote mmoja wetu. Wakaniuliza nikawaambia: ”Wagawanyeni na muwale. Kwani hakika mimi nadhani kuwa ni ruzuku ambayo Allaah amekuruzukuni.”

Yahyaa bin Ma´iyn amesema:

”Qur-aan ni maneno ya Allaah na haikuumbwa na imani ni maneno na vitendo, inazidi na inapungua.”

al-Husayn bin Fahm amesema:

“Nimemsikia Yahyaa bin Ma´iyn akisema: “Nilikuwa Misri pindi nilimuona kijakazi mmoja akiuzwa kwa dinari elfu. Sijapatapo kumuona mwanamke mrembo kama yeye. Allaah amswalie.” Ndipo nikasema: “Ee Abu Zakariyyaa! Hivi kweli mtu kama wewe unasema hivo?” Akasema: “Ndio. Allaah amswalie yeye na kila mwanamke mrembo.”

Yahyaa bin Sa´iyd amesema:

”Hatujapatapo kujiwa na mtu kama watu hawa wawili; Ahmad na Ibn Ma´iyn.”

Yahyaa bin Ma´iyn amesema:

”Sishangazwi na yule mwenye kukosea, isipokuwa yule asiyekosea.”

Yahyaa bin Ma´iyn amesema kuhusu mtu ambaye anaswali peke yake katika safu:

”Airudi swalah yake.”

Amesema juu ya imamu ambaye anawaswalisha watu pasi na wudhuu´:

“Hawatakiwi kuirudi swalah yake lakini yeye anatakiwa kuirudi.”

  • Mhusika: Imaam Shams-ud-Diyn Muhammad bin Ahmad adh-Dhahabiy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Siyar A´laam-in-Nubalaa’ (11/71-96)
  • Imechapishwa: 05/01/2021