Ili mtu aweze kupata fadhilah za usiku wa Qadr

Swali: Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ameufadhilisha mwezi wa Ramadhaan juu ya miezi mingine, nyusiku kumi za mwisho juu ya nyusiku zingine za mwaka na usiku wa Qadr ambao ni bora kuliko nyusiku elfu. Je, usiku wa Qadr umewekewa tarehe maalum au unakuwa ndani ya zile siku kumi za mwisho za mwezi mtukufu wa Ramadhaan?

Jibu: Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ameeleza ya kwamba usiku wa Qadr unakuwa katika zile siku kumi za mwisho za Ramadhaan na akabainisha (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) zile nyusiku za witiri zina uhakika zaidi kuliko zile nyusiku za shufwa. Kwa hivyo yule ambaye atasimama kuswali nyusiku zote basi ataupata usiku wa Qadr. Imesihi ya kwamba Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Yule atakayesimama kuswali usiku wa Qadr kwa imani na kwa matarajio, basi atasamehewa madhambi yake yaliyotangulia.”[1]

Maana yake ni kwamba yule ambaye atasimama kuswali na aina nyenginezo za ´ibaadah kama vile kusoma Qur-aan, kuomba du´aa, kutoa swadaqah na kadhalika hali ya kuamini kuwa Allaah ndiye ameyaweka hayo katika Shari´ah na kutaraji malipo kutoka Kwake – na si kwa ajili ya kujionyesha au malengo mengine miongoni mwa malengo mbalimbali ya kidunia – basi Allaah atamsamehe madhambi yake yaliyotangulia. Kikosi cha wanazuoni wengi wanaona kuwa haya yanapatikana kwa kujiepusha na madhambi makubwa. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Swalah tano, ijumaa moja mpaka nyingine na Ramadhaan mpaka Ramadhaan nyingine ni vyenye kufuta yaliyo kati yake midhali mtu atajiepusha na madhambi makubwa.”[2]

Tunamuomba Allaah awawafikishe waislamu wote kila maeneo kuweza kusimama hali ya kuamini na kutarajia malipo. Kwani hakika Yeye ni Mwingi wa kutoa, Mkarimu.

[1] al-Bukhaariy (1768) na Muslim (1268).

[2] Muslim (233).

  • Mhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Majmuu´-ul-Fataawaa (15/430)
  • Imechapishwa: 15/04/2023