Hukumu ya kuitikia adhaana inayotolewa kwenye redio

Swali: Je, inafaa kuitikia adhaana inayotolewa kupitia redio?

Jibu: Ikiwa ni katika wakati wa swalah basi imesuniwa kuitikia. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Mkimsikia muadhini basi semeni mfano wa anavosema, kisha niswalieni. Kwani hakika anayeniswalia mara moja basi Allaah humswalia mara kumi. Kisha niombeeni al-Wasiylah. Hakika hiyo ni ngazi Peponi ambayo haimstahikii isipokuwa mja miongoni mwa waja wa Allaah. Natumai kuwa mimi ndiye. Ambaye ataniombea kwa Allaah al-Wasilah basi umemthubutukia uombezi wangu.”

Ameipokea Muslim katika “as-Swahiyh” yake.

Vilevile amesema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Atakayesema wakati wa kusikia adhaana:

اللهم رب هذه الدعوة التامة والصلاة القائمة، آت محمداً الوسيلة والفضيلة، وابعثه مقاماً محموداً الذي وعدته

“Ee Allaah, Mola wa mwito huu uliotimia, swalah iliosimama, mpe bwana wetu Muhammad, al-Wasiylah na fadhilah na mfikishe daraja yenye kusifiwa ambayo umemuuahidi” basi utamthubutukia uombezi wangu siku ya Qiyaamah.”

Ameipokea al-Bukhaariy katika “as-Swahiyh” yake.

al-Bayhaqiy (Rahimahu Allaah) amezidisha kwa cheni ya wapokezi nzuri baada ya kumaliza kusema:

الذي وعدته إنك لا تخلف الميعاد

“… ambayo umemuuahidi. Kwani hakika wewe huendi kinyume na miadi.”

  • Mhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Majmuu´-ul-Fataawaa (10/363)
  • Imechapishwa: 30/09/2021