Je, kubaleghe ndio kikomo cha mtoto kuamrishwa kuswali?

Swali: Je, kubaleghe ndio kunazingatiwa kikomo cha mtoto kulazimishwa kutekeleza zile swalah zinazompita kutokana na sababu ya kulala au nyenginezo?

Jibu: Pindi mtoto wa kiume au wa kike atapobaleghe basi swalah, kufunga Ramadhaan na kufanya ´Umrah vitawalazimu wakiweza kufanya hivo. Watapata dhambi kwa kuyaacha na kwa kule kufanya kwao maasi. Hayo ni kutokana na kuenea kwa dalili za ki-Shari´ah.

Kubaleghe kunakuwa kwa kueneza miaka kumi na tano, kutokwa na manii kwa matamanio kwa kulala au akiwa macho na kuota nywele za sehemu ya siri. Kuna jambo la nne linaloongezeka kwa mtoto wa kike; nalo ni kupata hedhi.

Muda wa kuwa mtoto wa kiume au mtoto wa kike hajapata moja katika mambo haya, basi ´ibaadah hazijamuwajibikia. Lakini hata hivyo wanatakiwa kuamrishwa kuswali wanapokuwa na miaka saba na wapigwe kwa ajili yake wanapokuwa na miaka kumi. Aidha waamrishwe kufunga Ramadhaan na wahimizwe juu ya kila kheri kukiwemo kusoma Qur-aan, kuswali swalah za sunnah, kuhiji, kufanya ´Umrah, kusema “Subhaan Allaah”, “Laa ilaaha illa Allaah”, “Allaahu Akbar” na “Alhamduli Allaah”. Vilevile wakatazwe maasi yote. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Waamrisheni watoto wenu kuswali wanapokuwa na miaka saba  na wapigeni kwayo wanapofikisha miaka kumi na pia watenganisheni katika malazi.”

Isitoshe yeye (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alimkemea al-Hasan bin ´Aliy (Radhiya Allaahu ´anhumaa) kwa kula kutoka kwenye tende za swadaqah na akamwambia:

“Je, hukutambua kwamba swadaqah si halali kwetu?”

na akamwamrisha kutema tende ambayo alikuwa amechukua. Alipokuwa (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kipindi hicho alikuwa na miaka saba na miezi kadhaa.

  • Mhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Majmuu´-ul-Fataawaa (10/371)
  • Imechapishwa: 30/09/2021