´Allaamah ´Abdur-Rahmaan bin Naaswir as-Sa´diy (rahimahullaah) amesema:

Swali 8: Ni ipi hukumu ya muislamu mtenda dhambi?

Jibu: Yule mwenye kuamini na ni mwenye kumuabudu Allaah peke yake na wakati huo huo ni mwenye kuendelea katika maasi, ni muumini kwa ile imani alionayo na ni mtenda dhambi kutokana na yale mambo ya wajibu alioacha.

Imani yake ni pungufu. Anastahiki kulipwa kutokana na imani yake na kuadhibiwa kutokana na madhambi yake. Pamoja na hivyo hatodumishwa Motoni.

Imani kamilifu na iliotimia inamzuia mtu na kuingia Motoni.

Imani pungufu inamzuia mtu na kudumu Motoni.

MAELEZO

Yale yaliyothibitishwa na Shaykh katika swali hili ndio haki na ndio ´Aqiydah ya Ahl-us-Sunnah wal-Jamaa´ah tofauti na Murji-ah wanaosema kuwa imani haidhuriki kwa maasi.

Khawaarij na Mu´tazilah, waitwao pia “Waa´iydiyyah”, wanasema kwamba yule mwenye kufanya dhambi kubwa atadumishwa Motoni milele. Ahl-us-Sunnah wal-Jamaa´ah ni wenye kutofautiana na watu hawa katika suala hili.

Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala) amewasema vibaya watenda maasi na akawatishia juu ya maasi yao na madhambi yao makubwa. Amesema (Jalla wa ´Alaa):

إِنَّ الَّذِينَ يَأْكُلُونَ أَمْوَالَ الْيَتَامَىٰ ظُلْمًا إِنَّمَا يَأْكُلُونَ فِي بُطُونِهِمْ نَارًا ۖ وَسَيَصْلَوْنَ سَعِيرًا

“Hakika wale wanaokula mali ya mayatima kwa dhuluma, hapana shaka kwamba wanakula katika matumbo yao moto na watauingia moto uliowashwa vikali mno.”[1]

وَالسَّارِقُ وَالسَّارِقَةُ فَاقْطَعُوا أَيْدِيَهُمَا جَزَاءً بِمَا كَسَبَا نَكَالًا مِّنَ اللَّـهِ ۗ وَاللَّـهُ عَزِيزٌ حَكِيمٌ

“Mwizi mwanamume na mwizi mwanamke ikateni mikono yao – ni malipo kwa yale waliyoyachuma, ndio adhabu ya kupigiwa mfano kutoka kwa Allaah. Allaah ni Mwenye nguvu kabisa, Mwenye hekima ya yote.”[2]

الزَّانِيَةُ وَالزَّانِي فَاجْلِدُوا كُلَّ وَاحِدٍ مِّنْهُمَا مِائَةَ جَلْدَةٍ ۖ وَلَا تَأْخُذْكُم بِهِمَا رَأْفَةٌ فِي دِينِ اللَّـهِ إِن كُنتُمْ تُؤْمِنُونَ بِاللَّـهِ وَالْيَوْمِ الْآخِرِ ۖ وَلْيَشْهَدْ عَذَابَهُمَا طَائِفَةٌ مِّنَ الْمُؤْمِنِينَ

“Mzinifu mwanamke [asiyeolewa] na mzinifu mwanamme [asiyeoa], mpigeni kila mmoja katika wawili hao bakora mia na wala isiwashikeni kwa ajili yao huruma katika dini [kupitisha Shari’ah] ya Allaah mkiwa nyinyi mnamwamini Allaah na siku ya Mwisho. Na washuhudie adhabu yao [ya kupigwa mijeledi] kundi la waumini.”[3]

Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Hazini mwenye kuzini wakati anapozini hali ya kuwa ni muumini, haibi mwenye kuiba pindi anapoiba hali ya kuwa ni muumini, hanywi pombe mwenye kunywa pombe pindi anapokunywa pombe hali ya kuwa ni muumini, hapori mwenye kupora pindi anapopora, jambo linalofanya watu kumwangalia kwa ajili ya hilo, hali ya kuwa ni muumini.”[4]

Hiyo ina maana kwamba mzinifu, mnywaji pombe na mwizi hawana imani kamili. Anatoka katika imani na anabaki katika mzunguko wa Uislamu.

´Imraan bin Huswayn (Radhiya Allaahu ´anh) ameeleza kwamba mwanamke mmoja kutoka Juhaynah alikuja kwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ilihali amebeba mimba ya uzinzi. Akasema: “Ee Mtume wa Allaah! Nastahiki kuadhibiwa. Nisimamishie adhabu.” Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akamwita msimamizi wake na akasema: “Mtendee wema. Atakapozaa basi njoo naye.” Akafanya hivo ambapo Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akaamrisha mavazi yake yafungwe vizuri kisha akapigwa mawe. Baada ya hapo akamswalia swalah ya jeneza. ´Umar (Radhiya Allaahu ´anh) akasema: “Ee Mtume wa Allaah! Unamswalia ilihali amezini?” Akajibu: “Hakika ametubia tawbah ambayo lau ingeligawanywa kwa watu sabini al-Madiynah basi ingeliwaenea. Hivi kweli kuna tawbah bora zaidi ya kwamba ameipeleka nafsi yake mwenyewe kwa Allaah (Ta´ala)?”[5]

Zipo dalili nyingi zengine zinazoonyesha kuwa mwenye kufanya dhambi kubwa amesemwa vibaya na kulaumiwa kutokana na dhambi yake lakini hata hivyo bado ni muislamu na kunatarajiwa juu yake yale yanayotarajiwa kwa wapwekeshaji. Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala) amesema kuhusu muuaji:

فَمَنْ عُفِيَ لَهُ مِنْ أَخِيهِ شَيْءٌ فَاتِّبَاعٌ بِالْمَعْرُوفِ وَأَدَاءٌ إِلَيْهِ بِإِحْسَانٍ

“Anayesamehewa na nduguye kwa lolote basi kufuatilizwa kwake kuwe kwa wema na kumlipa kwake iwe kwa ihsani.”[6]

Amemwita kuwa ni ndugu yake pamoja na kwamba ni muuaji. Allaah (´Azza wa Jall) amesema:

وَإِن طَائِفَتَانِ مِنَ الْمُؤْمِنِينَ اقْتَتَلُوا فَأَصْلِحُوا بَيْنَهُمَا ۖ فَإِن بَغَتْ إِحْدَاهُمَا عَلَى الْأُخْرَىٰ فَقَاتِلُوا الَّتِي تَبْغِي حَتَّىٰ تَفِيءَ إِلَىٰ أَمْرِ اللَّـهِ ۚ فَإِن فَاءَتْ فَأَصْلِحُوا بَيْنَهُمَا بِالْعَدْلِ وَأَقْسِطُوا ۖ إِنَّ اللَّـهَ يُحِبُّ الْمُقْسِطِينَ إِنَّمَا الْمُؤْمِنُونَ إِخْوَةٌ فَأَصْلِحُوا بَيْنَ أَخَوَيْكُمْ ۚ وَاتَّقُوا اللَّـهَ لَعَلَّكُمْ تُرْحَمُونَ

“Ikiwa makundi mawili ya waumini yatapigana, basi suluhisheni baina yao. Lakini mojawapo likikandamiza jengine, basi piganeni na ambalo linakandamiza mpaka lielemee katika amri ya Allaah. Likishaelemea, basi suluhisheni kati yao kwa uadilifu na tendeni haki. Kwani hakika Allaah anawapenda wanaotenda haki. Hakika waumini ni ndugu, hivyo basi suluhisheni kati ya ndugu zenu na mcheni Allaah ili mpate kurehemewa.”[7]

Amewaita kuwa ni ndugu pamoja na kupigana kwao kati yao.

al-Bukhaariy amepokea katika “as-Swahiyh” kupitia kwa Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu ´anh) aliyesema:

“Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) aliletewa bwana mmoja mnywaji pombe. Akaamrishwa achapwe. Baadhi yetu wakampiga kwa mikono yao, wengine wakampiga kwa viatu vyao na wengine wakampiga kwa nguo zao. Alipoondoka zake mtu mmoja akasema: “Anani huyu? Allaah amtweze.” Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akasema: “Msiwe ni wasaidizi wa shaytwaan dhidi ya ndugu yenu.”[8]

Akamwita kuwa ni ndugu pamoja na kwamba ni chapombe.

Dalili hizi zinawasambaratisha Murji-ah wanaosema kuwa imani haidhuriki kwa maasi. Vilevile zinawasambaratisha Khawaarij na Mu´tazilah wanaosema kuwa watenda madhambi makubwa watadumishwa Motoni milele. Kuna dalili ngapi zilizopokelewa katika Sunnah zinazofahamisha kwamba wenye kufanya madhambi makubwa wataadhibiwa ndani ya Moto kisha baadaye wataondoshwa ndani yake na wataingizwa Peponi! Miongoni mwa dalili hizo ni yale yaliyopokea Abu Sa´iyd al-Khudriy (Radhiya Allaahu ´anh) aliyeeleza kuwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Watapoingia watu wa Peponi Peponi na watu wa Motoni Motoni Allaah atasema: “Yule ambaye moyoni mwake mlikuwa na imani sawa na mbegu ya hardali mwondosheni.” Watatolewa baada ya kuwa wamekwishachoma na kuwa makaa na wataingizwa kwenye mto wa Uhai. Kisha waanze kuchipuka kama inavyochipuka mbegu iliyobebwa na mafuriko.”[9]

Amesema  (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Hamuoni kuwa kunatoka manjano na yenye kupinda?”[10]

Katika upokezi wa Muslim imekuja:

“Pindi Allaah atapomaliza kuhukumu kati ya waja na akataka kuwaondosha Motoni wale anaotaka kuwaondosha kutokana na rehema Zake, atawaamrisha Malaika kumwondosha Motoni yule ambaye alikuwa hamshirikishi Allaah pamoja na chochote miongoni mwa wale waliokuwa wakisema ´hapana mungu wa haki isipokuwa Allaah` katika wale ambao Allaah anataka kuwarehemu. Watawatambua Motoni, watawatambua kwa athari ya sijda zao. Allaah (Ta´ala) ameuharamishia Moto kula athari ya Sujuud. Watatoka Motoni baada ya kuchomwa Motoni. Watamiminiwa maji ya Uhai ambapo wachipuke kama inavyochipuka mbegu iliyobebwa na mafuriko.”[11]

Kadhalika imetajwa katika Hadiyth zinazozungumzia uombezi ya kwamba atatolewa Motoni yule aliyesema ´hapana mungu wa haki isipokuwa Allaah` na moyoni mwake kulikuwa na imani sawa na mbegu kidogo, imani sawa na shayiri, imani sawa na mbegu ya hardali au imani sawa na mduduchungu[12]. Hadiyth zote hizi zimepokelewa kwa mapokezi kemkem na zinatupa faida kwamba watenda madhambi makubwa watatoka Motoni kwa uombezi wa waombezi na kwa sababu ya rehema ya Mwingi wa huruma.

Shaykh (Rahimahu Allaah) amesema:

“Imani kamilifu na iliotimia inamzuia mtu na kuingia Motoni.

Imani pungufu inamzuia mtu na kudumu Motoni.”

Haya yanathibitishwa na maneno ya Allaah (´Azza wa Jall):

الَّذِينَ آمَنُوا وَلَمْ يَلْبِسُوا إِيمَانَهُم بِظُلْمٍ أُولَـٰئِكَ لَهُمُ الْأَمْنُ وَهُم مُّهْتَدُونَ

“Wale walioamini na hawakuchanganya imani zao na dhuluma, hao ndio watakaopata amani nao ndio walioongoka.”[13]

Ni lazima kwenu, enyi waja wa Allaah, kushikamana na ´Aqiydah hii. Hii ndio ´Aqiydah ya Ahl-us-Sunnah wal-Jamaa´ah iliyojengeka juu ya dalili kutoka katika Qur-aan na Sunnah kwa mujibu wa uelewa wa Salaf.

[1] 04:10

[2] 05:38

[3] 24:02

[4] al-Bukhaariy (2475) na Muslim (57).

[5] Muslim (1696).

[6] 2:178

[7] 49:9-10

[8] al-Bukhaariy (6781)

[9] Ibn-ul-Athiyr amesema: ”Kama mapovu na udongo.” (an-Nihaayah (1/442)).

[10] al-Bukhaariy (6560) na Muslim (184).

[11] Muslim (182).

[12] al-Bukhaariy (44) na (3976).

[13] 06:82

  • Mhusika: ´Allaamah Ahmad bin Yahyaa an-Najmiy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Fath Rabb-il-Bariyyaat ´alaa Kitaab Ahamm-il-Muhimmaat, uk. 46-51
  • Imechapishwa: 30/09/2021