“Hatuna haja ya wanachuoni – Qur-aan na Sunnah vinatutosheleza”

Swali: Ni yapi maoni yako kwa mwenye kusema ya kwamba yeye anachukua elimu yake tu kutoka kwenye Qur-aan na Sunnah na hachukui kutoka kwa wanachuoni kwa kutumia hoja ya kwamba Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amekamilisha Dini.

Jibu: Ametakasika Allaah! Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ameamrisha kutafuta elimu kutoka kwa wanachuoni. Allaah (Jalla wa ´Alaa) Amesema:

فَاسْأَلُواْ أَهْلَ الذِّكْرِ إِن كُنتُمْ لاَ تَعْلَمُونَ

“Basi waulizeni wenye ukumbusho kama nyinyi hamjui.” (16:43)

Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Mwenye kupita njia ambapo anatafuta elimu basi Allaah Atamsahilishia njia ya kwenda Peponi.”

Hakusema akae nyumbani kwake na kusoma vitabu. Ni lazima apite njia, sawa ikiwa ni kwa kusafiri, kukaa pamoja na wanachuoni na vikao vya kielimu. Hizi ndio njia ya kusoma na za elimu. Sio miongoni mwa njia za kutafuta elimu kuchukua kitabu na kusoma na kudai ya kwamba kitabu hicho kinakutosheleza na umefahamu na mfano wa hayo. Hili ni kosa. Hizi sio miongoni mwa njia za kutafuta elimu. Njia hii wewe ndio umeizusha. Haizingatiwi kuwa ni miongoni mwa njia za kutafuta elimu.

Kitabu unatakiwa kukisoma kwa wanachuoni ili waweze kukufafanulia na kukubainishia nacho, yaliyo ya sahihi na yasiyokuwa ya sahihi.

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: http://www.alfawzan.af.org.sa/sites/default/files/al_makruf-14-08-1433.mp3
  • Imechapishwa: 15/06/2015