Hali tatu ambapo sio wajibu kuelekea Qiblah

Ni sharti kuelekea Qiblah. Kunavuliwa katika hilo mambo matatu:

1 – Ikiwa sio muweza. Kwa mfano mgonjwa aliyeelekeza uso wake Qiblah na hawezi kuelekea Qiblah. Katika hali hii kuelekea Qiblah kunamkatikia. Allaah (Ta´ala) amesema:

فَاتَّقُوا اللَّـهَ مَا اسْتَطَعْتُمْ

”Mcheni Allaah muwezavyo.”[1]

لَا يُكَلِّفُ اللَّـهُ نَفْسًا إِلَّا وُسْعَهَا

“Allaah hakalifishi nafsi yoyote isipokuwa kwa kadiri ya uwezo wake.” (02:286)

Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Nikikuamrisheni jambo, basi lifanyeni kadiri na muwezavyo.”[2]

2 – Ikiwa ni katika hali ya khofu kubwa. Kwa mfano mtu anapigwa vita na adui au anafukuzwa na moto unaotaka kumuunguza. Muhimu ni kwamba yuko katika khofu kubwa. Katika hali hii aswali kule amekoelekeza uso wake. Dalili ya hilo Allaah (Ta´ala) amesema:

فَإِنْ خِفْتُمْ فَرِجَالًا أَوْ رُكْبَانًا ۖ فَإِذَا أَمِنتُمْ فَاذْكُرُوا اللَّـهَ كَمَا عَلَّمَكُم مَّا لَمْ تَكُونُوا تَعْلَمُونَ

“Mkikhofu [adui basi swalini] hali mnatembea au mmepanda [kipando]. Mtakaokuwa katika amani mdhukuruni Allaah [swalini] kama alivyokufunzeni yale mliyokuwa hamyajui.” (02:239)

Maneno Yake (Ta’ala):

فَإِنْ خِفْتُمْ

“Mkiogopa… 

ni yenye kuenea na inahusu khofu zote. Maneno Yake (Ta’ala):

فَإِذَا أَمِنتُمْ فَاذْكُرُوا اللَّـهَ كَمَا عَلَّمَكُم مَّا لَمْ تَكُونُوا تَعْلَمُونَ

“Mtakapokuwa katika amani mdhukuruni Allaah [swalini] kama alivyokufunzeni yale mliyokuwa hamyajui.”

ni dalili yenye kuonyesha kuwa Dhikr yoyote anayoiacha mtu kwa ajili ya khofu hana dhambi juu yake. Katika hilo kunaingia kuelekea Qiblah.

Miongoni mwa dalili ya hilo vilevile ni pamoja na Aayah mbili tukufu na Hadiyth tulizotangulia kuzitaja zenye kuonyesha kuwa uwajibu umefungamana na uwezo.

3 – Swalah iliyopendekezwa katika safari. Mtu akiwa katika safari, ni mamoja akiwa ndani ya ndege, gari au mnyama, basi aswali popote uso wake ulipoelekea ikiwa ni swalah iliyopendekezwa. Kwa mfano Witr, Dhuhaa, kisimamo cha usiku na nyenginezo.

[1] 64:16

[2] al-Bukhaariy (7288).

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Riyaadh-is-Swaalihiyn (01/374-375)
  • Imechapishwa: 22/05/2023