Wanazuoni wengi wakaguzi wamethibitisha kwamba utaratibu wa ulinganizi unatakiwa uwe kwa mujibu wa Qur-aan na Sunnah na kwa mfumo wa kinabii. Miongoni mwa watu ambao wamelithibitisha hilo vyema zaidi na wakaingia kwa kina zaidi na wakajengea hoja kwa akili na nukuu ni Shaykh-ul-Islaam Ibn Taymiyyah (Rahimahu Allaah) ambaye aliulizwa swali lifuatalo:

Kikosi cha watu kinakusanyika juu ya madhambi makubwa, ikiwa ni pamoja na kuua, kupora, kuiba, kunywa pombe na mengineyo. Shaykh mmoja ambaye anatambulika kwa kheri na kufuata Sunnah akakusudia kuwakataza watu hao kutokamana na mambo hayo na hakuweza kuwafikia kwa njia nyingine isipokuwa kwa nyimbo na kwa nia hii. Kulipigwa matari na kukaimbwa mashairi yanayoruhusiwa pasi na vipengele vyovyote vya ujana. Baada ya yeye kufanya hivo vijana wengi walitubia. Matokeo yake akawa yule ambaye haswali wala hatoi zakaah na pia anaiba sasa anajiepusha na mambo yenye utata, anatekeleza mambo ya faradhi na anajiepusha na mmbo ya haramu. Je, inaruhusiwa kwa Shaykh huyu kuimba kwa njia hii kutokana na yale manufaa yanayopelekea katika jambo hilo na kwamba hawezi kuwalingania kwa njia nyingine isipokuwa hii tu?

Jibu: Himdi zote anastahiki Allaah, Mola wa walimwengu.

Msingi wa kujibu swali hili na mengine mfano wake, mtu anatambua kuwa Allaah amemtuma Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kwa uongofu na dini ya haki ili izishinde dini zingine zote. Aidha itambulike kuwa Allaah amemkamilishia yeye na Ummah wake dini. Amesema (Ta´ala):

الْيَوْمَ أَكْمَلْتُ لَكُمْ دِينَكُمْ وَأَتْمَمْتُ عَلَيْكُمْ نِعْمَتِي وَرَضِيتُ لَكُمُ الْإِسْلَامَ دِينًا

”Leo nimekukamilishieni dini yenu na nimekutimizieni neema Yangu na nimekuridhieni kwenu Uislamu uwe ndio dini yenu.”[1]

Yule mwenye kumtii amebashiriwa furaha, na yule mwenye kumuasi amebashiriwa kula khasara. Amesema (Ta´ala):

وَمَن يُطِعِ اللّهَ وَالرَّسُولَ فَأُوْلَئِكَ مَعَ الَّذِينَ أَنْعَمَ اللّهُ عَلَيْهِم مِّنَ النَّبِيِّينَ وَالصِّدِّيقِينَ وَالشُّهَدَاء وَالصَّالِحِينَ وَحَسُنَ أُولَئِكَ رَفِيقًا

“Atakayemtii Allaah na Mtume basi hao watakuwa pamoja na wale Allaah aliowaneemesha – Manabii na wakweli na mashahidi na waja wema – na uzuri ulioje kuwa na tangamano kama hili!”[2]

وَمَن يَعْصِ اللَّـهَ وَرَسُولَهُ فَإِنَّ لَهُ نَارَ جَهَنَّمَ خَالِدِينَ فِيهَا أَبَدًا

“Yeyote atakayemuasi Allaah na Mtume Wake, basi hakika atapata Moto wa Jahannam hali ya kudumu humo milele.”[3]

Amewaamrisha viumbe wakati wa kukhitilafiana kuhusu mambo ya dini basi warudishe katika yale aliyomtumiliza nayo. Amesema (Ta´ala):

فَإِن تَنَازَعْتُمْ فِي شَيْءٍ فَرُدُّوهُ إِلَى اللَّـهِ وَالرَّسُولِ إِن كُنتُمْ تُؤْمِنُونَ بِاللَّـهِ وَالْيَوْمِ الْآخِرِ ۚ ذَٰلِكَ خَيْرٌ وَأَحْسَنُ تَأْوِيلًا

”Mkizozana juu ya jambo, basi lirudisheni kwa Allaah na Mtume mkiwa mnamuamini Allaah na siku ya Mwisho. Hivyo ni bora na matokeo mazuri kabisa.”[4]

Allaah ameeleza kuwa yeye (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) analingania kwa Allaah na katika njia Yake ilionyooka:

قُلْ هَـٰذِهِ سَبِيلِي أَدْعُو إِلَى اللَّـهِ ۚ عَلَىٰ بَصِيرَةٍ أَنَا وَمَنِ اتَّبَعَنِي

“Sema: “Hii ndio njia yangu: nalingania kwa Allaah, juu ya ujuzi na umaizi – mimi na anayenifuata.”[5]

وَلَـٰكِن جَعَلْنَاهُ نُورًا نَّهْدِي بِهِ مَن نَّشَاءُ مِنْ عِبَادِنَا ۚ وَإِنَّكَ لَتَهْدِي إِلَىٰ صِرَاطٍ مُّسْتَقِيمٍ صِرَاطِ اللَّـهِ الَّذِي لَهُ مَا فِي السَّمَاوَاتِ وَمَا فِي الْأَرْضِ ۗ أَلَا إِلَى اللَّـهِ تَصِيرُ الْأُمُورُ

”… lakini tumeijaalia kuwa ni nuru, tunamwongoza kwayo Tumtakaye kati ya waja Wetu. Na hakika wewe bila shaka unaongoza kuelekea njia iliyonyooka – Njia ya Allaah ambaye ni Vyake pekee vyote vilivyomo mbinguni na vyote vilivyomo ardhini. Tanabahi! [Kuwa ni] kwa Allaah pekee yanaishia mambo yote.”[6]

Ameeleza kwamba yeye (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) anaamrisha mema, anakataza maovu, anahalalisha vilivyo vizuri na anaharamisha vilivyo vibaya:

وَرَحْمَتِي وَسِعَتْ كُلَّ شَيْءٍ ۚ فَسَأَكْتُبُهَا لِلَّذِينَ يَتَّقُونَ وَيُؤْتُونَ الزَّكَاةَ وَالَّذِينَ هُم بِآيَاتِنَا يُؤْمِنُونَ الَّذِينَ يَتَّبِعُونَ الرَّسُولَ النَّبِيَّ الْأُمِّيَّ الَّذِي يَجِدُونَهُ مَكْتُوبًا عِندَهُمْ فِي التَّوْرَاةِ وَالْإِنجِيلِ يَأْمُرُهُم بِالْمَعْرُوفِ وَيَنْهَاهُمْ عَنِ الْمُنكَرِ وَيُحِلُّ لَهُمُ الطَّيِّبَاتِ وَيُحَرِّمُ عَلَيْهِمُ الْخَبَائِثَ وَيَضَعُ عَنْهُمْ إِصْرَهُمْ وَالْأَغْلَالَ الَّتِي كَانَتْ عَلَيْهِمْ ۚ فَالَّذِينَ آمَنُوا بِهِ وَعَزَّرُوهُ وَنَصَرُوهُ وَاتَّبَعُوا النُّورَ الَّذِي أُنزِلَ مَعَهُ ۙ أُولَـٰئِكَ هُمُ الْمُفْلِحُونَ

”Rehema Yangu imekienea kila kitu. Basi nitawahukumia wale wenye kumcha Allaah na wanaotoa zakaah na ambao wao wanaziamini Aayah Zetu. Wale wanomfuata Mtume, Nabii asiyejua kuandika na kusoma, wanamkuta ameandikwa kwao katika Tawraat na Injiyl anawaamrisha mema na anawakataza maovu na anawahalalishia vizuri na anawaharamishia vibaya na anawaondoshea mizigo yao na minyororo iliyokuwa juu yao. Basi wale waliomwamini na wakamtukuza na wakamnusuru na wakafata Nuru ambayo imeteremshwa pamoja naye – hao ndio wenye kufaulu.”[7]

Allaah amemwamrisha Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) mema yote, akamkataza maovu yote, akahalalisha kila kilicho kizuri na akaharamisha kila kilicho kibaya. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

”Allaah hajapatapo kumtuma Mtume yeyote isipokuwa ilikuwa ni haki juu yake kuuelekeza Ummah wake katika kheri anayoifahamu juu yao na kuwaonya na shari anayoifahamu juu yao.”[8]

al-´Irbaadhw bin Saariyah (Radhiya Allaahu ´anh) amesema:

“Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alituwaidhi mawaidha ambayo nyoyo ziliingiwa na khofu kwayo na macho yakatokwa na machozi. Tukasema: “Ee Mtume wa Allaah! Ni kana kwamba ni mawaidha ya kutuaga, hivyo basi tuusie.” Akasema: “Nimekuacheni juu ya weupe ambao usiku wake ni kama mchana wake; hatopotea nayo isipokuwa mstahiki maangamivu. Hakika yule atakayeishi muda mrefu katika nyinyi basi atakuja kuona tofauti nyingi. Hivyo basi, lazimianeni na Sunnah zangu na Sunnah za makhaliyfah wangu waongofu na wenye kuongoza. Ziumeni kwa magego yenu. Na nakutahadharisheni na mambo yaliyozuliwa, kwani hakika kila kilichozuliwa ni Bid´ah.”[9]

Ibn Mas´uud (Radhiya Allaahu ´anh) amesimulia kuwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Eyi watu! Hakuna chochote kinachokuwekeni karibu na Pepo na kukuweni mbali na Moto isipokuwa nimekuamrisheni nacho, na hakuna chochote kinachokuwekeni mbali na Pepo na kukusogezeni karibu na Moto isipokuwa nimekukatazeni nacho.”[10]

 al-´Irbaadhw bin Saariyahamesimulia kuwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Nimekuacheni katika weupe; usiku wake ni kama mchana wake. Hakuna anayepotea humo isipokuwa anayestahiki kuangamia.”[11]

Kanuni hii tukufu na yenye kuenea imetajwa katika Qur-aan na Sunnah. Wanazuoni, akiwemo al-Bukhaariy na al-Baghawiy, wameiwekeakichwa cha khabari. Kwa hivyo yule anayeshikamana na Qur-aan na Sunnah basi ni katika mawalii wa Allaah na wenye kumcha, kundi lake lililofaulu na jeshi Lake lililoshinda. Salaf walikuwa wakisema:

“Sunnah ni kama safina ya Nuuh; yule mwenye kuipanda anaokoka na yule mwenye kubaki nyuma anazama.”

az-Zuhriy (Rahimahu Allaah) amesema:

“Wanazuoni wetu waliotangulia walikuwa wakisema: “Kushikamana na Sunnah ni kuokoka.”[12]

Yakishatambulika haya basi ni lazima yale ambayo Allaah anawaongoza kwayo wapotofu, anawaelekeza waliopotoka na anawasamehe watenda madhambi yawe katika ule ujumbe ambao amemtumiliza kwao Mtume Wake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) katika Qur-aan na Sunnah. Vinginevyo endapo ule ujumbe ambao Allaah amemtumiliza kwao Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) hautoshi kwa jambo hilo, basi dini ya Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ingelikuwa pungufu na yenye kuhitaji kukamilishwa.

Jengine mtu anatakiwa kujua kuwa matendo mema ambayo Allaah ameamrisha ima iwe kwa njia ya ulazima au kwa njia ya mapendekezo. Allaah amekataza pia matendo mabovu. Kama kitendo kimekusanya manufaa na madhara, hekima ya Mwekaji Shari´ah ni kwamba ikiwa manufaa yake yatashinda madhara yake, anakiweka kitu hicho katika Shari´ah, na ikiwa madhara yake yanashinda manufaa yake, hakiweki katika Shari´ah – kinyume chake anakikataza. Allaah (Ta´ala) amesema:

كُتِبَ عَلَيْكُمُ الْقِتَالُ وَهُوَ كُرْهٌ لَّكُمْ ۖ وَعَسَىٰ أَن تَكْرَهُوا شَيْئًا وَهُوَ خَيْرٌ لَّكُمْ ۖ وَعَسَىٰ أَن تُحِبُّوا شَيْئًا وَهُوَ شَرٌّ لَّكُمْ ۗ وَاللَّـهُ يَعْلَمُ وَأَنتُمْ لَا تَعْلَمُونَ

”Mmeandikiwa kupigana vita nako ni chukizo kwenu na huenda mkachukia jambo na hali lenyewe ni kheri kwenu na huenda mkapenda jambo na hali lenyewe ni la shari kwenu; na Allaah anajua na nyinyi hamjui.”[13]

يَسْأَلُونَكَ عَنِ الْخَمْرِ وَالْمَيْسِرِ ۖ قُلْ فِيهِمَا إِثْمٌ كَبِيرٌ وَمَنَافِعُ لِلنَّاسِ وَإِثْمُهُمَا أَكْبَرُ مِن نَّفْعِهِمَا

”Wanakuuliza kuhusu pombe na kamari. Sema: “Katika viwili hivyo mna dhambi kubwa na manufaa [fulani] kwa watu; na dhambi yake viwili hivyo ni kubwa kuliko manufaa yake.”[14]

Kwa ajili hiyo ndio maana Allaah (Ta´ala) akayaharamisha baada ya hapo.

Vivyo hivyo yale matendo ambayo watu wanaona kuwa yanawakurubisha mbele ya Allaahlakini Allaah na Mtume Wake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam)hawakuyaweka katika Shari´ah; ni lazima madhara yake yawe makubwa zaidi kuliko manufaa yake. Kwa sababu manufaa yake yangelikuwa makubwa zaidi kuliko madhara yake, basi Shari´ah isingeyapuuza. Yeye ni Mwingi wa hekima na hapuuzi manufaa ya dini na wala yale mambo ambayo yanawafanya waumini kuwa karibu na Mola wa walimwengu.

Shaykh aliyetajwa kushindwa kuwafanya watenda madhambi makubwa wakatubia isipokuwa kwa njia ya mfumo uliyozuliwa ambao umetajwa katika swali, ni dalili inayofahamisha kuwa Shaykh huyo ni mjinga wa mifumo iliyowekwa katika Shari´ah ambayo kwayo wanasamehewa watenda madhambi makubwa au mifumo hiyo imemshinda. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam), Maswahabah na wanafunzi wa Maswahabah walikuwa wakiwalingania walio waovu zaidi kuliko watu hawa – katika makafiri, watenda madhambi na maasi – na walifanya hivo kwa kutumia zile njia zilizowekwa katika Shari´ah. Allaah aliwatosheleza nazo kutokamana na mifumo iliyozuliwa. Haijuzu kusema kuwa Allaah hakumtuma Mtume Wake kwa mifumo iliyowekwa katika Shari´ah ambayo inaweza kuwafanya watenda madhambi wakatubia. Ni jambo linalotambulika vyema na kwa mapokezi mengi kwamba Allaah (Ta´ala) aliwasamehe makafiri wengi wasiohesabika kutokamana na ukafiri, ufuska na maasi kutokana na ile mifumo iliyowekwa katika Shari´ah ambayo haina hiyo mikusanyiko ya Bid´ah iliyotajwa. Bali wale wa awali waliotangulia, wale wahamaji na wanusuraji, na wale waliowafuata kwa wema, walitubu kwa Allaah (Ta´ala) kwa mifumo iliyowekwa katika Shari´ah na si kwa mifumo hii iliyozuliwa. Miji na vijiji vya waislamukatika nyakati zote imejaa watu waliotubu kwa Allaah na wakamcha Allaah na wakafanya yale mambo yanayopendwa na Allaah na kumfurahisha kwa kutumia njia zilizowekwa katika Shari´ah na si kwa njia hizi za Bid´ah.

Kwa hivyo haiwezekani kusema kwamba watenda maasi hawawezi kutubia isipokuwa kwa njia hizi za kizushi. Bali mtu anaweza kusema kuwa kuna Mashaykh ambao ni wajinga juu ya taratibu hizi zilizowekwa katika Shari´ah na zenye kuwashinda, hawana elimu ya Qur-aan na Sunnah na yale anayotakiwa kuwazungumzisha watu na kuwasikilizisha nayo katika yale ambayo Allaah hufanya akawasamehe kwayo, ambapo Shaykh huyu akapondoka kutokamana na njia zilizowekwa katika Shari´ah na badala yake akaziendea zile zilizozuliwa. Ima akafanya hivo kutokamana na nia njema – akiwa ni mtu wa dini – au ikawa lengo lake ni kutaka kuwa na utawala juu yao na kula mali zao kwa batili.”[15]

Baada ya hapo akasema:

“Muulizaji anauliza kama ni halali au haramu. Swali lenyewe ni la jumla na mkanganyiko na kwa ajili hiyo hukumu inaweza kuwa yenye kutatiza. Matokeo yake mtoa fatwa anashindwa kutoa jibu la uchambuzi juu ya swali hilo. Kwa sababu kusikiliza nyimbo kunaweza kuwa kwa njia mbili:

1 – Kwa lengo la kuburudika na pumbao, kama yanavofanya mengine yote yanayoziburudisha nyoyo, ijapo ndani yake kuna aina fulani ya pumbao na michezo, kama nyimbo za harusi.

2 – Kwa lengo la dini na ´ibaadah kwa ajili ya kuzirekebisha nyoyo, kuyapa nguvu mapenzi kwa Mola, kuzitakasa nyoyo, kuisafisha mioyo na kuzalisha ndani ya mioyo khofu, kujirejea, mapenzi, ulaini wa moyo na mengineyo katika aina za ´ibaadah na utiifu.

Kwa hiyo ni lazima kupambanua kati ya nyimbo za wenye kufanya ´ibaadah na nyimbo za wenyekutumbwiza, nyimbo zinazoimbwa na watu harusini, sherehe na ada nyinginezo za kimila na nyimbo zinazopitika kwa ajili ya kuzitengeneza nyoyo na kujikurubisha kwa Mola wa mbingu. Je, zinasikizwa kwa lengo la ´ibaadah? Je, ni njia ya kuweza kumfikia Allaah? Je, ni lazima kuzikiliza kwa sababu zinailainisha mioyo na malengo mengine? Ni kama ambavomanaswara wanaimba nyimbo hizi katika makanisa yao kwa lengo la ´ibaadah na utiifu na si kwa lengo la michezo na burudani.

Ukishayajua haya, basi swali linatakiwa kuwa kama inafaa kwa Shaykh kuyafanya mambo haya ambayo ima ni haramu, yanachukiza au yameibahishwa kuwa ni kumwabudu Allaah, kulingania kwa Allaah na kuwafanya watenda madhambi wakatubia, kuwaelekeza kwayo waliopotea na kuwaongoza kwayo wapotofu. Kama inavyotambulika dini ina misingi miwili. Hakuna dini isipokuwa ile iliyowekwa na Allaah katika Shari´ah na wala hakuna haramu isipokuwa ile iliyofanywa na Allaah kuwa haramu. Allaah (Ta´ala) amewasimanga washirikina kwa kule kuharamisha kwao yale ambayo hayakuharamishwa na Allaahna wakaweka Shari´ah ya dini ambayo Allaahhakuiidhinisha.”[16]

Haya ambayo Shaykh-ul-Islaam Ibn Taymiyyah (Rahimahu Allaah) ameyathibitisha hapa yako katika kilele cha juu cha uwazi na ubainifu. Uhalisia wa swali ni kama inafaa kwa Shaykh ambaye anataka kuwarekebisha watenda madhambi kutumia njia zozote ambazo zitamfikisha katika lengo hilo, ni mamoja ni za haramu, zinachukiza au zimeruhusiwa. Shaykh (Rahimahu Allaah) akasimamisha hoja za kukata kabisa kwamba njia zote ni haramu muda wa kuwa hazikuwekwa katika Shari´ah na haikuthibiti kuwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) aliitumia hata kama yenyewe kama yenyewe imeruhusiwa. Hilo ni kwa kulazimiana na msingi imara kwa Ah-us-Sunnah wal-Jamaa´ah: hatumwabudu mwingine isipokuwa Allaah na wala hatumwabudu isipokuwa kwa yale aliyotuwekea katika Shari´ah kupitia Mtume Wake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam).

[1] 5:3

[2] 4:69

[3] 72:23

[4] 4:59

[5] 12:108

[6] 42:52-53

[7] 7:156-157

[8] Muslim (1844).

[9] Abu Daawuud, at-Tirmidhiy, Ibn Maajah na Ibn Hibbaan katika ”as-Swahiyh”. at-Tirmidhiy amesema:

”Hadiyth ni nzuri na Swahiyh.”

Ni Swahiyh kwa mujibu wa al-Albaaniy katika ”Swahiyh-ut-Targhiyb wat-Tarhiyb” (37).

[10] al-Haakim (2/4), al-Bayhaqiy katika ”Shu´b-ul-Iymaan” (3/1458) na Sharh-us-Sunnah (14/303-305) ya al-Baghawiy.

[11] Ahmad (4/126), IbnMaajah (43) na al-Haakim (1/95).

[12] ad-Daarimiy katika ”as-Sunah”, al-Laalakaa’iy na al-Aajurriy katika ”ash-Shariy´ah”, uk. 314.

[13] 2:216

[14] 2:219

[15] Majmuu´-ul-Fataawaa (11/620-625).

[16] Majmuu´-ul-Fataawaa (11/631).

  • Mhusika: Shaykh ´Abdus-Salaam bin Barjas Aal ´Abdil-Kariym
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: al-Hujaj al-Qawiyyah ´alaa anna Wasaa-il-ad-Da´wah Tawqiyfiyyah, uk. 56-62
  • Imechapishwa: 22/05/2023