Amebahatisha Qiblah kisha imembainikia amekosea

Kuhusu asiyejua Qiblah kilipo, ni wajibu kwake kuelekea Qiblah. Lakini akijitahidi na kufanya bidii kisha baadaye ikambainikia amekosea baada ya kujitahidi, sio wajibu kurudi kuswali tena. Hatusemi kuwa kuelekea Qiblah kwa haki yake kunaanguka. Ni lazima kwake kuelekea Qiblah na ajitahidi kiasi na anavyoweza. Akijitahidi kiasi na anavyoweza kisha ikambainikia kuwa amekosea, harudi kuswali tena.Dalili ya hilo ni kwamba Maswahabah ambao walikuwa hawajui kuwa Qiblah kimegeuzwa kutoka Yerusalemu na kuelekea Ka´bah, siku moja walikuwa wanaswali Fajr katika msikiti wa Qubaa´ akawajia mtu na kuwaambia kuwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ameteremshiwa Qur-aan na kuamrishwa kuelekea Ka´bah, hivyo ielekeeni. Wakafanya hivo. Wakaielekea Ka´bah baada ya kuwa [walikuwa wanaswali ilihali] ilikuwa nyuma yao, wakawa wanaswali kwa kuielekea mbele. Wakaielekea na wakabaki katika swalah zao. Hili lilipitika katika zama za Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na hakuwakataza. Hivyo hilo linakuwa ni jambo lililowekwa katika Shari´ah. Mtu akikosea katika kuelekea Qiblah kwa kutokujua, harudi tena kuswali. Lakini pale itapombainikia, hata kama atakuwa ndani ya swalah, ni wajibu kwake kuelekea Qiblah. Tuseme kwa mfano mtu ameanza kuswali kinyume na Qiblah huku akifikiri kuwa ndio Qiblah na akaja mtu na kumwambia kuwa Qiblah kiko upande wa kulia au kushoto, ni wajibu kwake kuelekea upande wa kulia au wa kushoto pasina kuanza mwanzo. Kwa sababu ile sehemu yake ya mwanzo ilikuwa inatokamana na kujitahidi kwake na njia inayokubalika kwa mujibu wa Shari’ah, hivyo haibatiliki.

Kwa hivyo kuelekea Qiblah ni sharti miongoni mwa sharti za swalah. Swalah haisihi isipokuwa kwa kuelekea Qiblah isipokuwa katika hali tatu ambazo tumezitaja[1] au anapokosea mtu baada ya kujitahidi na kufanya lile analoweza.

[1] Tazama https://firqatunnajia.com/hali-tatu-ambapo-sio-wajibu-kuelekea-qiblah/

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Riyaadh-is-Swaalihiyn (01/375-376)
  • Imechapishwa: 22/05/2023