Hakujua kuwa swawm yake ya kulipa deni la Ramadhaan imeafikiana na Ramadhaan

Swali: Mtu akifunga swawm ya kulipa deni la Ramadhaan mwishoni mwa Sha´baan ambapo siku ya mwisho ya deni lake ikakutana na masiku ya Ramadhaan na bwana huyu hakujua kuwa Ramadhaan imeanza kwa sababu anaishi katika kijiji cha mbali – je, siku hii inazingatiwa kuwa amelipa deni au ametekeleza?

Jibu: Haisihi kuwa ni kulipa deni, utekelezaji wala swawm inayopendeza. Kusema kwamba haisihi kuwa ni kulipa deni wala swawm inayopendeza ni kwa sababu swawm ya Ramadhaan wakati wake ni mfinyu. ´Ibaadah zenye wakati mfinyu wakati wake hautoshi isipokuwa tu kwa yale yaliyowekewa Shari´ah. Amesema (Ta´ala):

فَمَن شَهِدَ مِنكُمُ الشَّهْرَ فَلْيَصُمْهُ

”Basi atakayeshuhudia miongoni mwenu mwezi [mpya] na afunge  swawm.”[1]

Amri inapelekea katika uwajibu. Kwa hivyo haijuzu kwa ambaye ´ibaadah inamuwajibikia kutekeleza swawm nyingine isiyokuwa hiyo.

Kusema kwamba haisihi utekelezaji ni kutokana na kwamba mfungaji amenuia swawm yake hii iwe ya Ramadhaan baada ya kupambazuka. Kwa hivyo haizingatiwi. Amesema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Hakuna swawm kwa ambaye hakulaza nia katika sehemu ya usiku.”

Kujengea juu ya hilo ni kwamba analazimika kulipa siku hiyo ya Ramadhaan ya mwaka huu. Kuhusu siku iliobakia ya Ramadhaan ya mwaka wa 1386 analazimika kuilipa. Ikiwa amechelewesha mpaka akafikiwa na Ramadhaan ya mwaka wa 1387 pasi na udhuru, basi mbali na kulipa kwa kufunga, analazimika vilevile kumlisha chakula masikini kwa kiasi cha Mudd ya ngano[2] kwa kila siku moja iliyompita. Lakini ikiwa alichelewesha kwa udhuru basi hakuna kinachomlazimu isipokuwa kulipa peke yake.

Muftiy wa Saudi Arabia

14/06/1388

[1] 02:185

[2] al-Fawzaan amesema:

”Kiwango cha Mudd ni gramu 563.” (Mukhtaswar Ahaadiyth-is-Swiyaam, uk. 52-53))

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Ibraahiym Aalush-Shaykh
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Majmuu´-ul-Fataawaa (04/202-203)
  • Imechapishwa: 24/03/2024