Hajaawirah wanaomtuhumu Mtume (عَلَيْهِ ٱلسَّلَامُ) kukosea

Swali: Kuna mwenye kusema kuwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) anakosea katika njia za Da´wah na ameshikilia maneno yake na anatolea dalili kwa kisa cha “´Abasa wa tawalla.”

Jibu: Tunamuomba Allaah afya. Hili ni suala la khatari sana kwa kumtuhumu nalo Mtume  (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ya kwamba anakosea katika njia za Da´wah au katika mambo ya Da´wah. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amekinga na kukosea.

Kuhusiana na suala la kipofu Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alikuwa na malengo. Wakati wakubwa wa washirikina walipomuomba aikae nao kikao maalum na wasiwepo waislamu madhaifu ndipo akapendelea kusilimu kwao na kuwaongoza. Haya ndio yalikuwa malengo ya Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Akataka kufanya waislamu madhaifu, kama Suhayb, ´Ammaar na Bilaal wawe na kikao kingine. Allaah akamkataza na hilo:

وَلَا تَطْرُدِ الَّذِينَ يَدْعُونَ رَبَّهُم بِالْغَدَاةِ وَالْعَشِيِّ يُرِيدُونَ وَجْهَهُ ۖ مَا عَلَيْكَ مِنْ حِسَابِهِم مِّن شَيْءٍ وَمَا مِنْ حِسَابِكَ عَلَيْهِم مِّن شَيْءٍ فَتَطْرُدَهُمْ فَتَكُونَ مِنَ الظَّالِمِينَ

“Na wala usiwafukuze wale wanaomwomba Mola wao asubuhi na jioni wanataka uso Wake. Si juu yako hesabu yao chochote na wala hesabu yako si juu yao chochote, hata uwafukuze, [kwani ukiwafukuza] utakuja kuwa miongoni mwa madhalimu.” (06:52)

Kisa cha ´Abasa ni kwamba ´Abdullaah bin Umm Maktuum, ambaye alikuwa kipofu na muadhini wa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam), alikuja na kutaka kumuuliza swali kipindi ambacho (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alikuwa na viongozi wa washirikina akiwazungumzisha na akiwalingania katika dini ya Allaah, Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) hakupendelea Ibn Umm Maktuum aje katika wakati huu na hakumjali kwa sababu alikuwa ni mwenye kushughulishwa na kuwazungumzisha watu hawa. Kwa ajili hii ndio maana Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala) akawa amemrekebisha kwa kitendo hicho. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alikuwa na malengo na nia ya kutaka kuwaongoza watu hawa na kuwalingania katika dini ya Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala).

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Duruus-ul-Haram http://www.alfawzan.af.org.sa/node/15216
  • Imechapishwa: 28/06/2020