Ahmad al-Ghumaariy amesema:

“Tambua kwamba Hadiyth zilizopokelewa juu ya watokaji ni zenye kufanana na Hadiyth za Khawaarij. Hata kama wote ni wenye kutoka katika dini (خوارج عن الدين) na wote ni mijibwa ya Motoni, kama alivosema Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam), pamoja na hivo wamegawanyika mafungu mawili:

1- Fungu la kwanza wanatambulika kwa jina hili. Wamesifiwa kuwa ni wenye kujikakama na kuchupa mpaka katika dini na kwamba mmoja wetu atazidharau swalah na swawm zake ukilinganisha na swalah na swawm zao.

2- Fungu la pili ni wale wapotofu wa sasa (au wakanamungu wa zama hizi?!?!) (ملاحدة العصر). Wamesifiwa kuwa wapumbavu na vijana na kwamba alama zao ni kunyoa upara.

Pindi kulipozuka pembe ya shaytwaan huko Najd mwishoni mwa karne ya kumi na fitina yake ikaenea, basi wanachuoni wote walikuwa wakizitumia Hadiyth hizi juu yake na wafuasi wake, kwa sababu kulikuwa hakujazuka aina ya Khawaarij hawa hapo kabla.”[1]

Mosi: Mapokezi yote kuhusu kuzuka kwa pembe ya shetani mashariki zimesimuliwa na ´Abdullaah bin ´Umar (Radhiya Allaahu ´anhumaa). Baadhi ya mapokezi yamefasiri wazi mashariki kwamba ni ´Iraaq. Hata hivyo yanavunjika matumizi ya wapotofu kwa watu walioko katika kisiwa cha kiarabu. Nitayataja mapokezi yote kutoka kwa Ibn ´Umar (Radhiya Allaahu ´anhumaa) kwa ajili ya kufichua batili iliyobebwa na mtunzi na watu wa mfano wake pindi anapowatuhumu batili watu wa nyanda za juu.

1- al-Bukhaariy, Muslim na Ahmad wamepokea kupitia kwa Naafiy´, kutoka kwa Ibn ´Umar (Radhiya Allaahu ´anh) ambaye ameeleza kuwa amemsikia Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akisema wakati alipokuwa ameelekea upande wa mashariki:

“Fitina itatokea hapo. Fitina itatokea hapo, ndiko kutakozuka pembe ya shaytwaan.”

Muslim amepokea kupitia kwa Naafiy´, kutoka kwa Ibn ´Umar ambaye ameleeza kuwa Mtume wa Allaah (Swalla Allahu ´alayhi wa sallam) alisimama pambizoni mwa mlango wa Hafswah na akashiria kwa mkono wake upande wa mashariki:

“Hapo ndio kutazuka fitina, hapo ndio kutatokea pembe ya shaytwaan.”

Alisema hivo mara tatu. ´Ubayd bin Sa´iyd (mmoja katika waalimu wa Muslim) amesema katika tamko lake:

“Mtume wa Allaah (Swalla Allahu ´alayhi wa sallam) alisimama pambizoni mwa mlango wa ´Aaishah.”

Upokezi wa Ahmad:

“Alisimama pambizoni mwa mlango wa ´Aaishah.”

2- Maalik, Ahmad na al-Bukhaariy wamepokea kutoka kwa ´Abdullaah bin Diynaar ambaye ameeleza kuwa amemsikia Ibn ´Umar akisema:

“Mtume wa Allaah (Swalla Allahu ´alayhi wa sallam) aliashiria upande wa mashariki na akasema: “Fitina itatokea kuaniza hapo. Fitina itatokea kuanzia hapo. Fitina itatokea kuanzia hapo, ndiko kutakozuka pembe ya shaytwaan.”

Ahmad, al-Bukhaariy, Muslim na at-Tirmidhiy wamepokea kupitia kwa az-Zuhriy, kutoka kwa Saalim, kutoka kwa baba yake aliyesimulia kuwa Mtume wa Allaah (Swalla Allahu ´alayhi wa sallam) alisimama karibu na mimbari na akasema:

“Fitina itatokea hapo. Fitina itatokea hapo. Fitina itatokea hapo, ndiko kutakozuka pembe ya shaytwaan.”

Katika upokezi wa al-Bukhaariy imekuja:

“Hapo ndiko kutatokea pembe ya jua.”

Katika upokezi wa Muslim imekuja:

“Fitina itatokea hapo. Fitina itatokea hapo. Fitina itatokea hapo, ndiko kutakozuka pembe ya shaytwaan.”

Katika upokezi wa at-Tirmidiy imekuja:

“Mtume wa Allaah (Swalla Allahu ´alayhi wa sallam) alisimama karibu na mimbari, akaashiria upande wa mashariki na kusema: “Huko ndio ardhi ya fitina, huko ndio kutazuka pembe ya shaytwaan (au pembe ya jua).”

at-Tirmidhiy amesema:

“Hadiyth hii ni nzuri na Swahiyh.”

3- Ahmad na Muslim wamepokea kupitia kwa Handhwalah, kutoka kwa Saalim, kutoka kwa Ibn ´Umar ambaye amesema:

“Mtume wa Allaah (Swalla Allahu ´alayhi wa sallam) aliashiria upande wa mashariki na akasema: “Fitina iko hapo. Fitina iko hapo, huko ndio kutazuka pembe ya shaytwaan.”

Hili ni tamko la Ahmad. Katika upokezi wake mwingine Ibn ´Umar amesema:

“Nilimuona Mtume wa Allaah (Swalla Allahu ´alayhi wa sallam) akiashiria kwa mkono wake ´Iraaq na akasema: “Fitina iko hapo. Fitina iko hapo, huko ndio kutazuka pembe ya shaytwaan.”

Cheni ya wapokezi wake ni Swahiyh. Wapokezi wake wote ni wapokezi wa al-Bukhaariy na Muslim.

Mapokezi yanayo faida ya wazi nayo ni kwamba fitina itatokea upande wa ´Iraaq na sio upande wa ardhi ya nyanda za juu za waarabu (نجد العرب). Yanawaraddi wapotofu wanaodai kuwa hadiyth zinalenga ardhi za waarabu.

4- Ahmad na Muslim wamepokea kupitia kwa ´Ikrimah bin ´Ammaar, kutoka kwa Saalim, kutoka kwa baba yake, kutoka kwa Ibn ´Umar ambaye amesema:

“Mtume wa Allaah (Swalla Allahu ´alayhi wa sallam) alitoka nje ya nyumba ya ´Aaishah na akasema: “Kichwa cha kufuru ni kuanzia hapa, ndio kutakozuka pembe ya shaytwaan.” Bi maana mashariki.”

5- Muslim amepokea kupitia kwa Ibn Fudhwayl, kutoka kwa baba yake aliyeeleza kwamba amemsikia Saalim bin ´Abdillaah bin ´Umar akisema:

“Enyi watu wa ´Iraaq! Ni mara  nyingi mnauliza juu ya dhambi ndogondogo na ni mara nyingi mnfanya dhambi kubwakubwa! Nimemsikia ´Abdullaah bin ´Umar akiseama: “Nimemsikia Mtume wa Allaah (Swalla Allahu ´alayhi wa sallam) akisema: “Fitina itakuja kutokea hapa, huko ndio kutatokea pembe ya shaytwaan” na akaashiria kwa mkono wake upande wa mashariki.” Mnakatana shingo zenu. Allaah amesema juu ya Muusa ambaye alimuua mmisri kwa kimakosa:

وَقَتَلْتَ نَفْسًا فَنَجَّيْنَاكَ مِنَ الْغَمِّ وَفَتَنَّاكَ فُتُونًا

“Ukaua mtu Tukakuokoa na janga na tukakujaribu majaribio mazito.”[2]

6- Ahmad, al-Bukhaariy na at-Tirmidhiy wamepokea kupitia kwa Ibn ´Awn, kutoka kwa Naafiy´, kutoka kwa Ibn ´Umar ambaye ameeleza kuwa Mtume wa Allaah (Swalla Allahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Ee Allaah! Tubarikie Shaam yetu! Ee Allaah! Tubarikie Yemeni yetu!” Wakasema: “Ee Mtume wa Allaah! Najd yetu!” Akasema: “Ee Allaah! Tubarikie Shaam yetu! Ee Allaah! Tubarikie Yemeni yetu!” Wakasema: “Ee Mtume wa Allaah! Najd yetu!” Nafikiri baada ya mara tatu alisema: “Huko kuna mitetemeko ya ardhi na huko kutatokea pembe ya shaytwaan.”

7- Ahmad amepokea kupitia kwa ´Abdur-Rahmaan bin ´Atwaa´, kutoka kwa Naafiy´, kutoka  kwa Ibn ´Umar aliyesimulia kuwa Mtume wa Allaah  (Swalla Allahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Ee Allaah! Tubarikie Shaam yetu! Ee Allaah! Tubarikie Shaam yetu!” Bwana mmoja akasema: “Na mashariki yetu, ee Mtume wa Allaah.” Akasema: “Huko ndio kutazuka pembe ya shaytwaan. Huko ndio kuna sehemu tisa ya kumi ya shari zote.”

Katika upokezi wa at-Twabaraaniy imekuja:

“Ee Allaah! Tubarikie Shaam yetu na Yemeni yetu!” Bwana mmoja akasema: “Na mashariki yetu, ee Mtume wa Allaah.” Akasema: “Ee Allaah! Tubarikie Shaam yetu na Yemeni yetu!” Bwana mmoja akasema: “Na mashariki yetu, ee Mtume wa Allaah.” Akasema: “Ee Allaah! Tubarikie Shaam yetu na Yemeni yetu! Ee Allaah! Hakika huko ndio kutazuka pembe ya shaytwaan. Huko ndio kuna sehemu tisa ya kumi ya kufuru zote na maradhi yasiyoponeka.”

8- Ahmad amepokea kupitia kwa Bishr bin Harb aliyeeleza kwamba amemsikia Ibn ´Umar akieleza kwamba amemsikia Mtume wa Allaah (Swalla Allahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Ee Allaah! Tubarikie Madiynah yetu, Swaa´ yetu na Mudd yetu, Yemeni yetu na Shaam yetu!” Kisha akaelekea mashariki na kusema: “Huko ndio kutazuka pembe ya shaytwaan, huko ndio kuna mitetemeko ya ardhi.”

9- Maalik ameeleza kuwa amefikiwa na khabari kuwa ´Umar bin al-Khattwaab (Radhiya Allaahu ´anh) alitaka kutoka kwenda ´Iraaq ambapo Ka´b bin al-Ahbaar akasema kumwambia:

“Usisafiri kwenda huko. Kwani hakika huko ndio kuna sehemu tisa ya kumi ya uchawi wote na kuna maradhi yasiyotibika.”

al-Khattwaabiy amesema:

“Pembe (القرن) ni kizazi cha watu wanaozuka baada ya kutokomea waliotangulia. Pembe ya nyoka (قرن الحية) ni kielezi cha matokeo mabaya.”[3]

Haafidhw Ibn Hajar amesema:

“Wengine wamesema kuwa kipindi hicho watu wa mashariki walikuwa makafiri ndio maana (Swalla Allahu ´alayhi wa sallam) akasema kuwa fitina itakuwa kutokea upande huo, jambo ambalo lilitokea. Fitina ya mwanzo ilikwua kutokea upande wa mashariki na hiyo ikawa ni sababu ya kufarikiana kwa waislamu. Shaytwaan anapenda na kufurahishwa na mambo kama hayo. Kadhalika Bid´ah ilizuka kutokea huko. al-Khattwaabiy amesema:

“Yule ambaye yuko Madiynah basi  nyanda zake za juu (نجد) ni pande za ´Iraaq na mazingira yake. Inazingatiwa ndio mashariki ya watu wa Madiynah. Najd maana yake ni nyanda za juu na ndio kinyume cha bonde (غور). Tihaamah yote ni katika bonde na Makkah ni katika Tihaamah.”

“Inapata kubainika kosa la Abu Daawuud wakati aliposema kuwa Najd ni pande za ´Iraaq kwa sababu inamfanya mtu kuelewa kwamba Najd ni maeneo maalum. Mambo sio hivyo. Bali kila eneo la ardhi lililoinuka kwa nisba ya pambizoni mwake kunaitwa “Najd” na mahali pa kinyume chake panaitwa “bonde” (غور).”[4]

[1] Mutwaabaqat-ul-Ikhtara´aat al-´Aswriyyah, uk. 76

[2] 20:40

[3] Fath-ul-Baariy (13/58).

[4] Fath-ul-Baariy (13/58).

  • Mhusika: ´Allaamah Hamuud bin ´Abdillaah at-Tuwayjiriy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Iydhwaah-ul-Mahajjah, uk. 132-138
  • Imechapishwa: 13/07/2020